Na, Mwandishi Wetu- Dar es Salaam

DAR ES SALAAM: SERIKALI imeendesha Zoezi la Kitaifa la Utayari na Kukabiliana na Maafa ya Mafuriko ya El Niño (SIMEX) kwa lengo la kupima ufanisi wa mifumo ya maandalizi, uratibu na mwitikio wa taasisi mbalimbali katika kukabiliana na maafa yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa nchini.

Zoezi hilo limejikita katika kuangalia athari za mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam, pamoja na athari zinazoweza kujitokeza katika mikoa ya Morogoro, Tanga na Mwanza.

Hayo yameelezwa leo, Novemba 19, 2026, na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, wakati akifungua semina hiyo.

Amesema mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuongeza vihatarishi vya maafa, ikiwemo mvua kubwa na mafuriko yanayoathiri maisha ya wananchi, shughuli za kiuchumi, miundombinu na huduma muhimu.

Ndagala alisema hali ya El Niño inaweza kuchangia kuongezeka kwa mvua na kuongeza hatari ya mafuriko katika baadhi ya maeneo nchini, hivyo kunahitajika maandalizi madhubuti na mipango iliyoratibiwa ili kuhakikisha taasisi zinakuwa na uwezo wa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.

“Zoezi hili si tu fursa ya kuonesha uwezo wa taasisi moja moja, bali muhimu zaidi ni kutathmini jinsi tunavyofanya kazi kwa pamoja kwa ufanisi kama mfumo mmoja ulioratibiwa wa kitaifa wa menejimenti ya maafa,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa vihatarishi vya maafa kupitia kuboresha maandalizi, mifumo ya tahadhari ya mapema, uratibu wa dharura na hatua za kukabiliana na maafa, kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa pamoja na mfumo wa kisheria.

Amewataka washiriki kutumia kikao hicho kubaini mapungufu na changamoto katika mifumo iliyopo, akieleza kuwa hatua.