Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU), huku maambukizi mapya yakipungua kwa kiwango kikubwa kutoka watu 98,754 mwaka 2010 hadi 33,511 mwaka 2025, hatua inayoongeza matumaini ya kufikia lengo la kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.
Mafanikio hayo yanaambatana na kupungua kwa vifo vinavyotokana na UKIMWI kutoka watu 55,833 hadi 25,995 katika kipindi hicho, huku maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yakishuka kutoka asilimia 9.1 hadi 6.2.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali kuimarisha huduma za kinga, upimaji, matibabu na matunzo, pamoja na ushirikiano na wadau mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Novemba 19, 2026, kuhusu Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu, Prof. Kabudi amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya utoaji huduma, kuongeza uwekezaji wa rasilimali za ndani na kushirikisha sekta binafsi ili kuhakikisha huduma za VVU na UKIMWI zinawafikia wananchi wote.
Amesema juhudi hizo zimeiwezesha Tanzania kupata mafanikio makubwa katika kufikia malengo ya kimataifa ya 95-95-95, yanayolenga kuhakikisha asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao za maambukizi, asilimia 95 ya wanaojua hali zao wanapata dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV), na asilimia 95 ya wanaotumia dawa hizo wanafubaza virusi mwilini.
Hata hivyo, Prof. Kabudi ametoa wito kwa vijana, hususan wenye umri wa miaka 15 hadi 24, kuongeza tahadhari na juhudi za kujikinga na VVU, kupima na kujua hali zao za afya, akieleza kuwa kundi hilo linachangia asilimia 33.3 ya maambukizi mapya, huku asilimia 77.7 ya maambukizi hayo yakitokea miongoni mwa vijana wa kike.
Amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuongeza elimu, huduma za kinga na juhudi zinazolenga vijana, hasa wasichana, ili kupunguza maambukizi mapya na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.
Akizungumzia Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani mwaka 2026, amesema yatafanyika kwa kaulimbiu isemayo, “Huduma Bora za Afya ni Msingi wa Kutokomeza UKIMWI, Tuendelee Kuimarisha Upatikanaji”, inayolenga kuhamasisha upatikanaji wa huduma, rasilimali na utashi wa kisiasa katika kuimarisha mwitikio wa Taifa dhidi ya VVU na UKIMWI.
Amesema maadhimisho hayo yataanza Novemba 24 hadi Desemba Mosi, 2026, katika kanda saba za Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), ambazo ni Mashariki, Kati, Ziwa, Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Magharibi na Kaskazini.
Aidha, amesema maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na kumbukumbu ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa TACAIDS mwaka 2001, ikiwa ni fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana, kubaini changamoto zilizopo na kuweka mikakati mipya ya kuimarisha mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

