Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amezitaka Taasisi zinazosimamia Haki Jinai zinazounda Utatu, kuendelea kuimarisha Mifumo ya Kidijitali kwenye Ushahidi na Usimamizi wa Mashauri ili taasisi hizo ziendelee kufanya kazi kwa ufanisi na ubora.

Mhe. Johari ameyasema hayo wakati Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Sita wa Taasisi zinazounda Utatu, Jijini Arusha tarehe 19 Novemba, 2026.

Akizungumza katika Mkutano huo, ambapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa mgeni rasmi, amesisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo inayosomana ili kurahisisha ufuatiliaji wa utendaji, pia uwepo wa mifumo hiyo utasaidia kuboresha ubadilishanaji wa taarifa na ufuatiliaji wa mashauri.

“Ushahidi wa kidijitali unaweza kuongeza thamani na kuaminika kwenye vyombo vya maamuzi vya utoaji haki, hivyo, imarisheni ukusanyaji, uhifadhi na mnyororo wa utunzaji wa Ushahidi.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha, Mhe. Johari amemshukuru, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa dhamira yake ya dhati ya kuimarisha mfumo wa haki jinai nchini.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pia amesisitiza juu ya umuhimu wa kuongeza kasi ya upelelezi na uendeshaji wa Mashtaka ikiwa ni pamoja na kuboresha ushirikiano baina ya taasisi hizo na kuwezesha mashtaka kuendeshwa katika ubora na kasi zaidi kwani ushahidi ukikusanywa kwa ubora unatoa hakikisho la kuwa na matokeo chanya na ya Haki.

Vilevile, Mhe. Johari amewataka washiriki wa Mkutano huo kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu, nidhamu, weledi na kutanguliza uzalendo kwa taifa, pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi.

”Taasisi zetu ni lazima zilinde uhuru wa Taifa, amani, usalama, utaratibu wa kikatiba na ustawi wa wananchi”. Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ameeleza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kutoa ushauri wa kisheria na kushirikiana na Taasisi hizo katika kushughulikia changamoto za kisheria zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mkutano Mkuu wa Sita wa Taasisi zinazosimamia Haki Jinai, zinazounda Utatu unahusisha washiriki kutoka *Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Uhamiaji, Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Nchini na Jeshi la Polisi.

Mkutano Mkuu wa Sita wa Taasisi zinazosimamia Haki Jinai, zinazounda Utatu 2026 umebeba kauli mbiu isemayo *Ushirikiano wa Wadau Dhidi ya Uhalifu: Tanzania Salama Kuelekea Dira 2050*