Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Salum Mnuna, ameitaka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuimarisha mikakati ya kupunguza upotevu wa maji na kuboresha miundombinu ya utoaji huduma ili kuongeza upatikanaji na uhakika wa huduma hiyo kwa wananchi.

Mnuna ametoa msisitizo huo leo Novemba 19, 2026, alipokutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, katika kikao kilicholenga kujadili utekelezaji wa mikakati ya kupunguza upotevu wa maji pamoja na kuboresha miundombinu ya huduma za maji.

Amesema ni muhimu kwa DAWASA kuendelea kutekeleza mikakati hiyo kwa ufanisi ili kuboresha utendaji wa mamlaka hiyo, kuongeza upatikanaji wa maji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika na endelevu.

Aidha, Mnuna amesema kikao hicho kimejadili umuhimu wa kutumia teknolojia katika shughuli za utafutaji, uchakataji na uwasilishaji wa taarifa, akieleza kuwa matumizi sahihi ya teknolojia yatasaidia kuongeza ufanisi na kuboresha mifumo ya utendaji katika utoaji huduma za maji.

“Tumejadili pia umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika utafutaji, uchakataji na uwasilishaji wa taarifa, jambo ambalo litaongeza ufanisi katika utendaji,” amesema Mnuna.

Ameeleza kuwa EWURA, katika kutekeleza jukumu lake la kudhibiti sekta ya maji nchini, inaendelea kusimamia utendaji wa mamlaka za maji ikiwemo DAWASA ili kuhakikisha zinafuata viwango na masharti yaliyowekwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa usimamizi huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji zilizo endelevu na zinazotolewa kwa gharama stahiki, sambamba na kuimarisha ufanisi wa mamlaka zinazohusika na utoaji wa huduma hiyo.