Na WMJJWM- Morogoro
Amani na usalama kwa wanawake ni jambo muhimu linalopaswa kuzingatiwa katika kufikia maendeleo endelevu ya Taifa.
Hayo yamesemwa Novemba 19, 2026, mkoani Morogoro na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Yahaya Mmbaga, wakati akizungumza na Kikosi Kazi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kinachofanya maandalizi ya taarifa za mipango kazi ya kisekta kwa ajili ya kuandaa taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama (2025–2029).
Mmbaga amesema wanawake ni miongoni mwa makundi yanayoathirika na migogoro ya aina mbalimbali katika jamii, hivyo ni muhimu kuhakikisha migogoro inazuiliwa kuanzia ngazi ya familia, jamii hadi Taifa ili kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo bila hofu wala wasiwasi.
“Athari ya migogoro katika jamii, huwafikia Wanawake zaidi, hivyo ni muhimu kuhakikisha ujenzi wa dhana ya amani na usalama kwa wanawake unapewa kipaumbele ikiwemo uzingatiaji wa maoni yao katika shughuli za maendeleo ya jamii, uongozi na Uchumi shirikishi, amesema” Mmbaga.
Ameeleza kwamba, lengo la maandalizi ya taarifa hiyo ni kuimarisha uratibu wa utekelezaji, ufuatiliaji wa maendeleo na utoaji wa taarifa kuhusu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama.
Aidha, mpango kazi huo unalenga kuhakikisha wanawake na wanaume wanashiriki katika hatua zote za kuzuia na kutatua migogoro, ujenzi wa amani pamoja na masuala ya ulinzi na usalama.
Kwa upande wake, Afisa Mchambuzi wa Sera na Uratibu wa Masuala ya Amani na Usalama kwa Wanawake kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), Adolphina Emmanuel, amesema utekelezaji wa programu za wanawake, amani na usalama unapaswa kuleta matokeo yaliyokusudiwa na manufaa halisi kwa walengwa.
Akifafanua baadhi ya matokeo yanayotarajiwa, Adolphina amesema ni kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi, hususan katika masuala yanayohusu usalama, pamoja na kujenga na kuandaa viongozi wanawake wa baadaye kwa kuanza kuwawezesha wasichana tangu hatua za awali.
Amesema uwekezaji huo utasaidia kuandaa kizazi kijacho cha wanawake wenye uelewa na uwezo wa kushiriki katika masuala ya amani na usalama katika jamii zao.
Kikao kazi hicho kinafanyika kwa ushirikiano wa Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na ubalozi wa Ireland nchini, ambapo kwa awali unahusisha jumla ya mikoa sita ya Tanzania bara na Mikoa Miwili kutoka Zanzibar.

