Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamsaka dereva wa bajaji ambaye jina lake na anuani yake bado havijafahamika, kwa kusababisha ajali iliyopelekea majeruhi kwa abiria mmoja pamoja na uharibifu wa chombo hicho na kukimbia eneo la tukio.
Ajali hiyo imetokea Novemba 16, 2026, majira ya saa 02:30 usiku, katika barabara ya Uru Mawela, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo dereva wa bajaj ambaye, alikuwa akiendesha bajaji yenye namba za usajili MC 321CWM aina ya TVS akitokea Moshi kuelekea Uru Mawela, alishindwa kuimudu bajaji hiyo na kuacha njia na kutumbukia kwenye mtaro wa maji uliopo pembeni mwa barabara na dereva huyo kukimbia.
Katika ajali hiyo, abiria aliyefahamika kwa jina la Silvin Peter Kiwale alipata majeraha na kupewa fomu ya PF3 kabla ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa Mawenzi kwa ajili ya matibabu ambako alifariki dunia akiwa anaendelea na matibabu.
Chanzo cha awali cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva katika kukwepa mashimo barabarani na kusababisha bajaj kuacha njia na kutumbukia mtaroni. Chombo hicho kimehifadhiwa katika Kituo cha Polisi kwa ajili ya ukaguzi na hatua nyingine za kisheria.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa madereva wote wa vyombo vya moto kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, kuwa makini wanapokutana na changamoto za barabarani na kuhakikisha wanatoa taarifa kwa vyombo husika pale ajali inapotokea badala ya kutoroka eneo la tukio.
