Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Baraka Mesiaki akizungumza kwenye baraza hilo.jijini Arusha
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Baraka Mesiaki, amewataka viongozi na watendaji wa halmashauri hiyo kuongeza kasi ya uwajibikaji na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kupata huduma bora kutokana na halmashauri hiyo kuwa chombo chao cha maendeleo.
Mesiaki amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji AUWSA kuandaa mpango mkakati wa haraka na endelevu wa kukabiliana na changamoto ya maji yenye kiwango kikubwa cha floridi, ili wananchi waweze kupata maji safi na salama yanayokidhi mahitaji yao
Mesiaki ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kilichokuwa na ajenda mbalimbali zinazohusu utendaji wa Halmashauri, changamoto za wananchi na mwelekeo wa maendeleo ya eneo hilo
Aidha, ameitaka AUWSA kufuatilia kwa karibu maeneo ambayo huduma ya maji imekuwa haitolewi kwa uhakika, akisisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha maji yanapatikana kwa wakati na kuondoa usumbufu unaowakabili wananchi.
Katika sekta ya elimu, Mesiaki amemtaka Mkurugenzi kufuatilia mchakato wa usajili wa Shule ya Seliani na Sekondari ya Manyire ili ziweze kupata usajili unaotakiwa na kutambulika rasmi katika Mkoa wa Arusha.
Amesema halmashauri inapaswa kuhakikisha watoto wote wanaofikia umri wa kuanza elimu ya awali, msingi na kidato cha kwanza wanapata nafasi za kujiunga na shule, akieleza kuwa elimu ni haki ya msingi ambayo kila mtoto anapaswa kuipata.
Akizungumzia suala la maadili, Mesiaki amewataka wazazi kuimarisha malezi kwa kuwa karibu na watoto wao na kufuatilia mienendo yao, akionya kuwa mmomonyoko wa maadili unaendelea kuathiri heshima na misingi ya familia katika jamii.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa miradi yote ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika halmashauri hiyo, akiwataka watendaji kuhakikisha miradi inayotumia fedha za ndani inafuatiliwa kwa karibu ili kukamilika kwa wakati na kutoa matokeo yaliyokusudiwa.
Maelekezo hayo yametolewa katika kipindi ambacho Halmashauri ya Wilaya ya Arusha inaendelea kujadili suala la kupandishwa hadhi, huku ikielezwa kuwa imefanikiwa kushika nafasi ya tano kitaifa na ya pili kimkoa katika tathmini iliyotajwa.
