Na Mwandishi wetu, Nzega
MKUU wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, Naitapwaki Lemea Tukai amewapongeza wahitimu wa mafunzo ya jeshi la akiba maarufu kama mgambo kwenye Kata ya Itobo.
DC Tukai akizungumza na wahitimu hao baada ya kukagua gwaride la mwendo wa haraka na mwendo wa pole na kusikiliza risala yao, amewapongeza kwa kukamilisha mafunzo yao.
Amewaasa wahitimu hao kutumia vyema mafunzo hayo ikiwemo ukakamavu na nidhamu wanapokuwa na jamii inayowazunguka katika wilaya hiyo.
Amewaagiza waendelee kuwa na nidhamu katika maisha yao kwani wao ni jeshi la akiba lenye kuhitajika na linalokuwa na uangalizi katika eneo hilo.
“Hatutarajii kuona au kusikia eti wahitimu hawa ndiyo wanakuwa wanavunja sheria, au kuwa wakatili mitaani au walevi, laa ninyi ni jeshi la akiba mnapaswa kuyaishi mliyojifunza na kuhitimu,” amesema DC Tukai.
Hata hivyo, amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo wa eneo hilo wenye kuhitaji huduma za ulinzi wa maeneo yao ya kiuchumi kuwapa kipaumbele wahitimu hao kuliko wale ambao hawajapata mafunzo.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo ya jeshi la akiba kwenye Kata ya Itobo wamefurahia kuhitimu vyema mafunzo hayo.
Wameeleza kwamba wataendelea kutekeleza yale yote waliyofanya na kufundishwa na wakufunzi wao ikiwemo kuishi kikakamavu na kusaidia jamii inayowazunguka.
