Naibu Katibu Mkuu wizara ya fedha ,CPA Elijah Mwandumbya wakati akifungua Mkutano huo jijini Arusha leo

Mtendaji Mkuu wa IRMT ,Christopher Njovu akizungumza kwenye mkutano huo jijini Arusha

………..
Na Happy Lazaro, Arusha
WADAU wa usimamizi wa vihatarishi katika taasisi za umma na sekta binafsi wametakiwa kuongeza juhudi katika kubaini, kutathmini na kuweka mikakati ya kukabiliana na vihatarishi vinavyoweza kuathiri utendaji wa taasisi na ukuaji wa uchumi wa taifa.
Wito huo umetolewa jijini Arusha leo na Naibu Katibu Mkuu wizara ya fedha ,CPA Elijah Mwandumbya wakati akifungua Mkutano mkuu wa tisa wa mwaka wa wadau wa wasimamizi wa vihatarishi Tanzania unaowakutanisha wadau na wataalamu wa eneo hilo kwa ajili ya kujadili changamoto na kubadilishana uzoefu.
CPA Mwandumbya amesema usimamizi wa vihatarishi ni sehemu muhimu ya shughuli za kila siku za taasisi, hivyo maafisa wanaohusika na kubaini, kushauri na kusimamia mikakati ya kukabiliana na viatarishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Amesema wataalamu hao wana nafasi kubwa katika kuzisaidia taasisi kuwa imara na kujiandaa kukabiliana na changamoto mbalimbali, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza uwezo katika maeneo yanayoweza kuchochea utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumzia vihatarishi vinavyoathiri uchumi wa dunia, amesema janga la COVID-19, vita kati ya Urusi na Ukraine pamoja na mvutano wa Mashariki ya Kati vimeonesha namna matukio ya kimataifa yanavyoweza kuvuruga shughuli za kiuchumi, upatikanaji wa bidhaa muhimu na kuongeza gharama za maisha.
Amefafanua kuwa, Tanzania imeendelea kuchukua hatua za kupunguza athari hizo, huku akibainisha kuwa akiba ya fedha za kigeni nchini inatosha kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.3, kiwango kilicho juu ya kiwango cha chini kinachohitajika cha miezi minne.
Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea na shughuli za biashara, uwekezaji, kilimo, madini na utalii, huku wakizingatia viatarishi vinavyoweza kuathiri shughuli zao, ikiwemo magonjwa ya mlipuko kama Ebola katika nchi jirani.
Kwa upande wake,Mtendaji Mkuu wa IRMT ,Christopher Njovu amesema mkutano huo una malengo makuu matatu ambayo ni kubadilishana uzoefu, kuongeza maarifa na kujenga uwezo wa wataalamu katika masuala ya usimamizi wa viatarishi.
Amesema ajenda kuu zitakazojadiliwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kwa uchumi, akitolea mfano tahadhari ya uwezekano wa kutokea kwa El Nino ambayo inahitaji taasisi mbalimbali kujiandaa mapema ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Njovu amefafanua kuwa teknolojia na usalama wa mifumo ya kidijitali ni eneo jingine muhimu litakalojadiliwa kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mitandao, ambayo pamoja na kurahisisha utendaji imekuwa chanzo cha viatarishi vinavyoweza kusababisha upotevu wa fedha na taarifa za taasisi.
Amesema kuwa, washiriki watajadili athari za vita na migogoro ya kimataifa katika upatikanaji wa malighafi na bidhaa muhimu, akisisitiza kuwa taasisi zinapaswa kuwa na mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo ili zisikwamishe utekelezaji wa mipango na malengo yao.
