📌Asisitiza kuhusu ushiriki wa Watanzania katika sekta

Dar es Salaam

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuimarisha usimamizi wa shughuli za mafuta na gesi nchini, sambamba na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo.

Dkt. Homera ametoa maelekezo hayo leo Novemba 16, 2026, wakati akifungua Kikao cha Sita cha Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi la PURA kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Homera amesema Tanzania inapaswa kuendelea kutumia rasilimali zake za gesi asilia kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi na taifa, huku ikiendana na mwelekeo wa dunia wa matumizi ya nishati safi na salama kwa mazingira.

Aidha, ameitaka PURA kushirikiana na taasisi nyingine za sekta ya nishati katika kutekeleza ajenda ya mpito wa nishati, pamoja na kutumia fursa zinazotokana na biashara ya kaboni na teknolojia za ukamataji na uhifadhi wa hewa ukaa (Carbon Capture and Storage – CCS).

Dkt. Homera ameipongeza PURA kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi, hususan ushauri wa kitaalamu uliowezesha Serikali kutoa leseni nne za utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika vitalu vya Lindi-Mtwara, Eyasi-Wembere, Songo Songo Magharibi na Mnazi Bay Kaskazini.

Pia, amepongeza ushiriki wa PURA katika utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima 

vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay, ambao umechangia ugunduzi wa futi za ujazo bilioni 223 za gesi asilia katika kisima cha KASA-1X, pamoja na kuongeza uzalishaji wa gesi kutoka katika visima vingine vya eneo hilo.

 Mradi huo umewezesha ajira kwa Watanzania takribani 350 na kutoa zabuni zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 20 kwa watoa huduma wa ndani.

Katika hatua nyingine, Waziri Homera amesema ni muhimu kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu katika shughuli zote za mkondo wa juu wa petroli.

Hivyo ameitaka PURA kukamilisha na kuwasilisha Wizarani mkakati maalumu wa kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli ifikapo Desemba 31, 2026, kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais, Mhe.Deogratius Ndejembi wakati wa hafla ya kukabidhi leseni kwa TPDC.

Kuhusu uongezaji wa ujuzi kwa watumishi, Dkt. Homera amesema Wizara ya Nishati inaendelea kushughulikia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya mafunzo ya watumishi wa PURA na Wizara kwa ujumla, ili kuwawezesha kuongeza ujuzi na uwezo wa kitaalamu katika kutekeleza majukumu yao.