Mkurugenzi wa Bodi ya Chama cha Wanataaluma wa Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania (TPPA) Rachel Magege akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha
………..
Na Happy Lazaro, Arusha
Wanataaluma kutoka kada mbalimbali nchini wametakiwa kuzingatia sheria na taratibu za ukusanyaji, utunzaji na uchakataji wa taarifa binafsi ili kuzuia uvujaji na matumizi yasiyo sahihi ya taarifa zinazoweza kuhatarisha usalama na haki za wananchi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Bodi ya Chama cha Wanataaluma wa Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania (TPPA) Rachel Magege wakati akizungumza katika mafunzo ya ulinzi wa taarifa binafsi yaliyoandaliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) jijini Arusha.
Magege amesema amefurahishwa na mwaliko wa TLS wa kushiriki katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika Hoteli ya Lush Garden, akieleza kuwa ni muhimu kwa wanataaluma kuelewa wajibu wao katika kulinda taarifa binafsi wanazozipata wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa mawakili, maafisa wa serikali na washiriki wengine kuhusu umuhimu wa ulinzi wa taarifa binafsi, pamoja na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kukusanya, kuhifadhi na kuzitumia taarifa hizo.
Magege ameongeza kuwa taarifa binafsi zinapaswa kulindwa kwa sababu zinaweza kuibiwa, kutumika kinyume na madhumuni yaliyokusudiwa, kuchakatwa vibaya au kupotea, hali inayoweza kusababisha madhara kwa wahusika.
Amesisitiza kuwa matumizi yasiyo sahihi ya taarifa hizo yanaweza kuathiri haki na usalama wa mtu husika, hivyo kila taasisi na mtaalamu anayehusika na taarifa za watu anapaswa kuhakikisha anazisimamia kwa kuzingatia taratibu zinazotakiwa.
“washiriki wa mafunzo hayo wanatarajiwa kwenda kutumia maarifa waliyoyapata katika maeneo yao ya kazi, taasisi wanazozihudumia na hata katika maisha yao binafsi ili kujenga utamaduni wa kulinda taarifa za watu wengine.”amesema Magege.
Akifafanua umuhimu wa kuwapatia mafunzo hayo mawakili, Magege amesema TLS ina jukumu kubwa katika kuhudumia wananchi, kushirikiana na taasisi za umma na kutetea haki za watu, hivyo mawakili wanapaswa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kulinda taarifa wanazokabidhiwa na wateja wao.
Amesema taaluma ya sheria inahusisha upatikanaji na matumizi ya taarifa nyingi za watu, jambo linalofanya ulinzi wa taarifa binafsi kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya mawakili.
“Tanzania ina Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi iliyopitishwa mwaka 2022, ambayo imeweka msingi wa kisheria katika kusimamia namna taarifa binafsi zinavyokusanywa, kuhifadhiwa na kuchakatwa nchini.”amesema Magege.
Ameeleza kuwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi iliyoanzishwa mwaka 2024 imekuwa ikifanya kazi ya kutoa elimu kwa wananchi, taasisi na wadau mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria hiyo na kulinda taarifa za watu.
Hata hivyo, amesema ulinzi wa taarifa binafsi bado unakabiliwa na changamoto kubwa nchini kutokana na uelewa mdogo wa sheria hiyo kwa wananchi na baadhi ya taasisi, hali inayochangia kutokuzingatiwa ipasavyo kwa taratibu za usimamizi wa taarifa hizo.
Ameongeza kuwa changamoto hizo zinaonekana zaidi katika hatua za ukusanyaji, utunzaji na uchakataji wa taarifa binafsi, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili kuongeza uelewa kuhusu wajibu na haki zinazohusiana na taarifa hizo.
Magege amesisitiza kuwa mafunzo kwa wanataaluma ni hatua muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, huku akitoa wito kwa washiriki kwenda kuyatumia maarifa waliyoyapata kuhakikisha taarifa za watu zinakusanywa, zinatunzwa na kutumika kwa usahihi na kwa kuzingatia sheria.
Mkurugenzi wa Bodi ya Chama cha Wanataaluma wa Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania (TPPA) Rachel Magege akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha
