Antalya Uturuki, Na Mwandishi wetu

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amesema Tanzania imefungua imefungua Kituo cha Majadiliano (Negotiation Center) kwa ajili ya vijana wa Afrika.

Amesema hayo wakati akizungumza na Vijana wa Kitanzania na Nchi zingine jijini Antalya, Uturuki pembezoni mwa Mkutano wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP31 katika jengo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 14,2026 ikiwa ni siku maalum ya Vijana kulingana na ratiba za COP31.

Dkt. Muyungi aliwapongeza vijana hao kwa kukutana na kufanya Majadiliano ya pamoja na kuwafahamisha kuwa kituo hicho kimeanzishwa kwa ajili ya vijana wote wa Afrika hivyo aliwasisitiza vijana wote kukitumia kituo hicho kikamilifu. 

“Nafasi ya vijana katika majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi ni kubwa na kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuwaunga mkono,” alisema Dkt. Muyungi.

Kwa upande wake Mdau na Mtaalamu wa Mazingira anayeongoza Vijana, Bi. Sarah Pima alisema, Siku ya Vijana imekuwa yenye hamasa, mijadala mafunzo na makubaliano ya pamoja.

“Kwetu sisi siku hii tumeiadhimisha katika Jengo la Tanzania kwa kufanya vikao mbalimbali vilivyowakutanisha watoto kutoka nchi 14, pamoja na vijana kutoka Afrika na nje ya Afrika. Katika mkutano huo tumejadili ajenda muhimu,” alisema.

Alitaja agenda hizo kuwa ni Maandalizi kuelekea COP32, Namna ya kufanya kazi pamoja na kuunganisha sauti zetu kama vijana, Njia za kupata fedha kwa ajili ya hatua za mabadiliko ya tabianchi na mijadala mingine yenye tija kwa mustakabali wetu. 

Alisems siku hiyo ilihitimishwa kwa sherehe maalum iliyowakutanisha wadau mbalimbali na vijana kutoka mataifa tofauti tofauti,” alisema Bi. Sarah huku akiongeza kuwa maadhimisho ya siku ya vijana katika Mkutano wa COP31 yamethibitisha wazi kuwa Sauti ya vijana ni nguvu ya mabadiliko.