Na Mwandishi Maalumu, Morogoro
Wananchi wa Tarafa ya Mikese Wilaya ya Morogoro Vijijini wanufaika na huduma za uchunguzi, elimu na matibabu ya magonjwa ya moyo zinazotolewa bure na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamisi Shaban Taletale.
Huduma hizo zinatolewa katika kambi maalumu iliyofunguliwa rasmi na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro Robert Mwega ambaye ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuungana na mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki kufikisha huduma adhimu kwa wananchi wa Tarafa ya Mikese.
Mwega alisema Mhe. Hamisi Taletale anasimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma bingwa za moyo kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza huduma hizo kusogezwa karibu na wananchi kuboresha afya na ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamisi Shaban Taletale alisema kambi hiyo imepangwa kufanyika katika Tarafa tatu zilizopo katika jimbo lake kuwawezesha wananchi wa jimbo hilo kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo bila gharama..
Aidha Mhe. Taletale alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge kwa kupokea ombi lake na kuwezesha upatikanaji wa madaktari bingwa kutoka katika Taasisi hiyo na kuwahudumia wananchi kwa moyo wa kujitolea.
Akielezea huduma za dawa zinazotolewa katika kambi hiyo mfamasia kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Baraka Mosi alisema wananchi wanapewa ushauri wa kitaalamu kuhusu matumizi sahihi ya dawa hususan wale ambao tayari wanatumia dawa mbalimbali
Baraka alisema elimu hiyo inahusisha maelekezo kuhusu namna sahihi ya kutumia dawa, madhara yanayoweza kujitokeza pamoja na namna bora ya kuhifadhi dawa, pia alisema JKCI imeenda na dawa za kutosha ili watu wote watakaohitaji dawa kupitia kambi hiyo waweze kuzipata kwa urahisi.
Naye mkazi wa Tarafa ya Mikese aliyepata huduma katika kambi hihyo Muharami Kagoda aliema huduma zinazotolewa katika kambi hiyo zimewagusa wananchi wa hali ya chini na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Muharami alisema huduma hizo ni msaada mkubwa kwa wananchi hususan wale wenye uwezo mdogo wa kiuchumi ambao wanapata changamoto ya kumudu gharama za matibabu, hivyo upatikanaji wa huduma hizo bure umewajengea wananchi imani na kuwapa nafasi ya kupata huduma za kitaalamu ambazo kwa baadhi yao zingekuwa vigumu kuzimudu.
Kambi ya matibabu katika Tarafa ya Mikese ni mwendelezo wa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa y moyo zilizoanza katika Tarafa ya Ngerengere na kuhamia Mikese ikiwa ni sehemu ya ushirikiano kati ya JKCI na Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki katika kusogeza huduma za kibingwa na bobezi karibu na wananchi.
