Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Ndugu Bakari Machumu, pamoja na viongozi mbalimbali wakizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe15 Novemba, 2026, kuhusu mafanikio ya Ziara ya Kikazi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Antalya nchini Uturuki ambapo alishiriki katika Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), pamoja na mikutano ya pembezoni ya Ngazi za Juu kuhusu masuala ya Nishati Safi ya Kupikia.
Ushiriki wa Tanzania katika COP31 nchini Uturuki, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, umeimarisha nafasi ya Taifa kimataifa na kufungua fursa za biashara, uwekezaji, nishati safi, teknolojia na ajira.
…………..
Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
ZIARA ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Uturuki na kushiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), imeiwezesha Tanzania kupata fursa za ufadhili wa miradi ya maji yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 120 na uwekezaji wa zaidi ya Dola milioni 150 katika sekta ya kilimo.
Matokeo hayo ni miongoni mwa mafanikio ya ziara hiyo iliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kuvutia mitaji na kutafuta rasilimali za kutekeleza miradi ya maendeleo, hususan katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 15, 2026, jijini Dar es Salaam kuhusu matokeo ya ziara hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, amesema ziara hiyo imefungua fursa za uwekezaji, biashara na ushirikiano na washirika wa maendeleo katika sekta mbalimbali.
Amesema kupitia mkutano wa COP31, Rais Samia alitumia jukwaa hilo kutetea haki ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea, akisisitiza kuwa Afrika inachangia kwa kiwango kidogo katika mabadiliko ya tabianchi, lakini inaendelea kukabiliwa na athari zake.
Machumu amesema ziara hiyo pia imeweka msisitizo katika kuimarisha sekta ya nishati, ambapo upatikanaji wa umeme nchini umeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 66, huku wadau wakisaidia zaidi ya shule 200 katika mikoa 31.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Richard Muyungi, amesema Mfuko wa Kimataifa wa Tabianchi (GCF) umekubali kutoa fedha zilizobaki kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji katika maeneo ya Ziwa Victoria na Simiyu, unaogharimu Dola za Marekani milioni 120.
Amesema mradi huo unatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 50,000 kwa kusafirisha maji umbali wa zaidi ya kilomita 25 na kuhudumia vijiji 103 mkoani Simiyu.
Dkt. Muyungi amesema Tanzania pia imepata fursa ya uwekezaji wa zaidi ya Dola milioni 150 katika sekta ya kilimo, utengenezaji wa bidhaa viwandani, misitu na usambazaji, kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa ziara hiyo imefungua njia ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mafunzo kuhusu mabadiliko ya tabianchi barani Afrika, huku Dar es Salaam ikitajwa kuwa eneo la kuanzisha kituo cha vijana kinachohusishwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Naye Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Tanzania inaendelea kutafuta fedha za kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC), ambao unahitaji Dola za Marekani milioni 19.3, ambapo tayari Dola milioni 7.3 zimepatikana na Dola milioni 12 zinahitajika.
Amesema Serikali inaendelea kushirikiana na mifuko ya kimataifa na taasisi za fedha kupata fedha hizo, ikiwamo kuhamasisha matumizi ya hati fungani za kijani ili kuwezesha utekelezaji wa miradi inayozingatia uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe, amesema Rais Samia alikutana na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, Novemba 12, ambapo walijadili masuala ya biashara, uwekezaji, ajira na utalii.
Amesema Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuelekeza juhudi katika kuongeza thamani ya biashara kati ya nchi hizo kutoka Dola za Marekani milioni 354 hadi kufikia Dola bilioni moja, huku Tanzania ikilenga kupanua soko la chai, kahawa, korosho, pamba, bidhaa za viwandani na madini.
Ameongeza kuwa katika mkutano huo, zaidi ya washirika 20 wa maendeleo walionesha utayari wa kuunga mkono juhudi za Tanzania katika nishati safi kwa shule na vituo vya afya, huku Rais Samia akisisitiza lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Naye Waziri wa Nishati, Juma Homera, amesema ziara hiyo imeongeza fursa za ushirikiano katika uwekezaji wa nishati jadidifu na upatikanaji wa fedha za kijani, huku Serikali ikiendelea kuhamasisha matumizi ya magari yanayotumia umeme na gesi ili kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuimarisha ukuaji wa uchumi.

