Na Mwandishi Wetu – Geneva, Uswisi

Tanzania imekubali mapendekezo 196 kati ya 280 yaliyotolewa na nchi mbalimbali katika Duru ya Nne ya Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR), hatua inayoonesha dhamira ya Serikali kuendelea kuimarisha ulinzi na utekelezaji wa haki za binadamu, utawala bora na maendeleo jumuishi, kwa kuzingatia Katiba, sheria na vipaumbele vya Taifa.Katika mapendekezo hayo yaliyotolewa katika Kikao cha 53 cha Kikundi Kazi cha Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, kilichofanyika Geneva, Uswisi, Tanzania haijaunga mkono mapendekezo 68, huku ikiahirisha kutoa msimamo kuhusu mapendekezo 16 ili kupata nafasi ya kuyafanyia uchambuzi na mashauriano zaidi kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.

Akitangaza matokeo hayo hivi karibuni jijini Geneva, Uswisi, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Ulega, amesema maamuzi yaliyofikiwa yanaonesha utayari wa Tanzania kuendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kukuza na kulinda haki za binadamu, huku ikiheshimu mamlaka yake ya kitaifa katika kuamua masuala yanayohusu mustakabali wa nchi.

Amesema mapendekezo 196 yaliyokubaliwa yanaendana na Katiba, sheria, sera na mipango ya maendeleo ya Taifa, hususan Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030, ambayo inaweka mkazo katika maendeleo jumuishi, ulinzi wa haki na ustawi wa wananchi.

“Mapendekezo yaliyokubaliwa yanahusu kuimarisha utawala bora, utawala wa sheria, upatikanaji wa haki, mageuzi ya kikatiba na huduma za msaada wa kisheria; kulinda haki za wanawake, watoto, watu wenye ulemavu ikiwemo wenye ualbino; pamoja na kuboresha huduma za elimu, afya, maji safi na salama na hifadhi ya jamii,” amesema Mhe. Ulega.Ameongeza kuwa mapendekezo mengine yanahusu utunzaji wa mazingira, kuimarisha ushirikiano na mifumo ya kimataifa na kikanda ya haki za binadamu, pamoja na kuhakikisha maendeleo yanawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi wala kumwacha mtu nyuma.

Akifafanua sababu za kutounga mkono mapendekezo 68, Waziri Ulega amesema baadhi ya mapendekezo hayo hayawiani na misimamo na vipaumbele vya kitaifa, hususan yanapogusa masuala yanayohusiana na mila, desturi, tamaduni na maadili ya jamii ya Kitanzania.

Amesema pia yapo mapendekezo yanayohitaji kuzingatia mazingira ya kikatiba, kisheria, kijamii na kiuchumi ya nchi, huku mengine yakihitaji utafiti, tathmini na mashauriano zaidi kabla ya kufikiwa kwa maamuzi.

Miongoni mwa maeneo ambayo Tanzania haikuunga mkono ni masuala ya mahusiano ya jinsia moja, kuondoa adhabu ya kifo, pamoja na mapendekezo yanayohitaji maamuzi kabla ya kukamilika kwa mashauriano ya kitaifa na mapendekezo ya kurekebisha matakwa ya kisheria ambayo kwa tathmini ya Serikali tayari yanaendana na viwango vya kimataifa.

Katika hatua nyingine, Serikali imeahirisha kutoa msimamo kuhusu mapendekezo 16 ili kufanya uchambuzi na mashauriano zaidi kuhusu athari zake za kisheria, kisera na kiuchumi, pamoja na mahitaji ya rasilimali fedha na watu yatakayohitajika katika utekelezaji wake.

Waziri Ulega, amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa maamuzi yatakayofikiwa yanazingatia uhalisia wa mazingira ya nchi, uwezo wa utekelezaji na kuepusha athari zisizotarajiwa.

Mapendekezo hayo yanahusu taratibu za dhamana, muda wa kushikiliwa kwa watuhumiwa na mfumo wa elimu bila ada, ambao Serikali inaendelea kuutekeleza.

Tanzania inatarajia kuwasilisha msimamo wake wa mwisho kuhusu mapendekezo hayo 16 katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachotarajiwa kufanyika Februari 2027, baada ya kukamilisha mashauriano na taasisi husika, zikiwemo Mahakama, Bunge, asasi za kiraia na wadau wengine, kwa kuzingatia mamlaka na majukumu yao ya kikatiba na kisheria.