Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Rugangira,akizungumza kwenye baraza hilo wilayani Arumeru

Mkurugenzi Mtendaji, Seleman Msumi, akizungumza kwenye baraza hilo jijini Arusha.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Baraka Mesiaki akizungumza kwenye baraza hilo

………..
Na Happy Lazaro, Arusha
Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha umeelekeza nguvu katika kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuboresha huduma kwa wananchi na kusukuma mbele mchakato wa kuipatia Halmashauri hiyo hadhi ya Manispaa.
Masuala hayo yameibuka katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kilichokuwa na ajenda mbalimbali zinazohusu utendaji wa Halmashauri, changamoto za wananchi na mwelekeo wa maendeleo ya eneo hilo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Rugangira, amesisitiza umuhimu wa kushughulikia suala la mita 100 pamoja na kuendelea na taratibu za kubadilisha hadhi ya Halmashauri kuwa Manispaa ili kuendana na mahitaji ya ukuaji wa eneo hilo.
Katika kusimamia uwajibikaji, Rugangira amewataka watumishi wa umma kutimiza wajibu wao kwa uadilifu na kuacha vitendo vya uzembe vinavyowasababishia wananchi usumbufu.
Aidha ameonya kuwa watakaobainika kutowajibika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji, Seleman Msumi, amesema wamepata mafanikio katika miradi mbalimbali ya maendeleo, akitaja nafasi ya tano kitaifa waliyoipata katika utekelezaji wa miradi ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2026.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Emmanuel Severe, amesisitiza umuhimu wa viongozi na watumishi kuwa karibu na wananchi badala ya kusubiri malalamiko yafike kwenye vikao, akiwataka kufika katika maeneo yao na kutafuta majibu ya changamoto zinazowakabili.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Baraka Mesiaki, ameeleza kuridhishwa na ushirikiano uliopo baina ya madiwani, mbunge, viongozi na watumishi, akiwashukuru kwa mchango wao katika kusukuma mbele shughuli za maendeleo na huduma kwa jamii.
Katika tukio jingine lililopambwa na mafanikio ya michezo, Baraza limetambua mchango wa timu za Halmashauri zilizoshiriki mashindano ya SHIMISEMITA 2026 yaliyofanyika Mbeya, ambapo timu ya mpira wa mikono ilitwaa nafasi ya pili kitaifa kati ya Halmashauri 177.
Kutokana na matokeo hayo, wachezaji na wadau waliofanikisha ushiriki wa timu hizo wamekabidhiwa vyeti vya pongezi, huku kombe waliloshinda likiwasilishwa mbele ya Baraza kama sehemu ya kutambua mafanikio hayo.
