Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay akizungumza kwenye baraza hilo jijini Arusha. 

………….. 

Happy Lazaro, Arusha.

Arusha. Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay ameahidi kufuatilia changamoto ya eneo la mita 200 linalohusisha Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na Jiji la Arusha, ili kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi kwa maslahi ya wananchi.

Akizungumza baada ya kushiriki kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Dkt. Lukumay amesema atafuatilia suala hilo kwa kushirikiana na mamlaka husika, akieleza kuwa ni sehemu ya wajibu wake wa kuwasemea na kutetea maslahi ya wananchi.

Amesema ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kwa utendaji wake, huku akimpongeza Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, pamoja na Mkurugenzi kwa usimamizi mzuri wa shughuli na rasilimali za halmashauri, ambao umechangia kupatikana kwa hati safi.

Dkt.Lukumay amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo katika Jimbo la Arumeru Magharibi, ikiwemo miundombinu ya barabara, maji, umeme na elimu.

“Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraja yaliyokuwa kero kwa wananchi, akitolea mfano daraja la Mirongoine na daraja la Oljoro kuelekea mnadani pamoja na kivuko cha Mwandeti .

Akizungumzia miundombinu ya barabara, amesema ujenzi wa barabara ya Mianzini–Ngaramtoni unaendelea vizuri kutokana na mkandarasi kufanya kazi kwa kasi, huku akibainisha kuwa malipo kwa mkandarasi huyo yamefanyika ili kurahisisha utekelezaji wa mradi.

Amesema katika sekta ya umeme, vijiji vyote 67 vya jimbo hilo tayari vimefikiwa na huduma hiyo, huku kazi ikiendelea kusambaza umeme katika vitongoji vichache vilivyosalia.

Katika sekta ya elimu, amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kujenga madarasa na kuhakikisha watoto wanapata fursa ya kusoma kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita, sambamba na kuwawezesha vijana kupata mikopo ya elimu ya juu na vyuo vya kati.

Lukumay amesisitiza umuhimu wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na ushirikiano na sekta binafsi, akieleza kuwa uwekezaji huo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa wananchi.

Ameongeza kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeipa sekta binafsi nafasi kubwa katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya nchi, ambapo takribani asilimia 70 ya uwekezaji unaolenga kufikia uchumi wa dola trilioni moja unatarajiwa kutoka sekta hiyo.

Ameitaja Taasisi ya TAHA kuwa miongoni mwa wadau wanaochangia maendeleo ya kilimo na upatikanaji wa maji kwa ajili ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikisha wadau hao katika kuimarisha uchumi wa wananchi.