Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kampasi ya Lindi, huku akipongeza hatua iliyofikiwa na usimamizi mzuri wa mradi huo.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais amepokelewa na Mkuu wa Chuo hicho na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda. Viongozi wengine ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Prof. Rose Acen Upor, na Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET wa UDSM, Prof. Liberato Venant Haule.

Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi, Prof. Haule amesema utekelezaji wa awamu ya kwanza umefikia asilimia 98, huku kampasi hiyo ikitarajia kudahili wanafunzi 360 kuanzia Machi 2027.

Amesema kampasi hiyo itaanza kutoa mafunzo ya ngazi za astashahada na stashahada katika maeneo ya uzalishaji na uchakataji wa mazao ya kilimo na mifugo.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa na kukagua ujenzi, Makamu wa Rais amepongeza usimamizi wa mradi huo, unaotekelezwa kupitia Mpango wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Aidha, ameielekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuangalia uwezekano wa kuipa kipaumbele Kampasi ya Lindi katika awamu ya pili ya HEET, hususan ujenzi wa nyumba za walimu na wafanyakazi.