
Aagiza barabara ya Kibena–Kidegembye ipewe kipaumbele katika kusaini mikataba
Azindua jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Njombe
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema bei ya ununuzi wa mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imefikia shilingi 500 kwa kilo, kufuatia majadiliano ya Serikali yaliyolenga kushughulikia malalamiko ya wakulima kuhusu bei ndogo.
Amewataka wakulima ambao bado wana mahindi kutumia fursa ya bei hiyo kuuza mazao yao.
“Niliitisha tena kikao na sasa tumekubaliana kwamba bei iwe 500,” amesema.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Novemba 14, 2026), wakati akizungumza na kusikiliza kero za wananchi katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Kidegembye, Jimbo la Lupembe, Mkoani Njombe.
Amesema Wizara ya Kilimo ilieleza changamoto ya kuwa na mahindi mengi yaliyonunuliwa msimu uliopita, lakini aliitaka kuzingatia pia wakulima waliokuwa na mavuno mengi yanayohitaji soko.
Waziri Mkuu pia amesema Serikali imeelekeza kuharakishwa kwa usafirishaji wa pembejeo kwenda mkoani Njombe. Amesisitiza maandalizi ya mapema kuhusu pembejeo na majadiliano ya bei za mazao ili kupunguza changamoto zinazoweza kuwasababishia wakulima hasara.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ameitaka Wizara ya Ujenzi kuipa kipaumbele sehemu ya Kibena–Kidegembye, katika barabara ya Kibena–Lupembe–Madeke, itakapoanza kusaini mikataba ya miradi ambayo taratibu zake za manunuzi zimekamilika.
“Tutakapoanza tu kusaini miradi hii ambayo ilikuwa inasubiria kusainiwa, mradi huu wa barabara hii uwe kipaumbele,” amesema.
Ameshauri, ikiwezekana, mkataba huo usainiwe Lupembe ili wananchi washuhudie hatua hiyo, baada ya kusubiri ujenzi kwa muda mrefu.
Akijibu hoja ya Mbunge wa Lupembe, Edwin Enosy Swalle, Waziri Mkuu amesema kuchelewa kwa mradi huo hakukutokana na kutofuatiliwa na Mbunge au uzembe wa watendaji, bali uamuzi wa Serikali wa kutanguliza kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Amesema Serikali ilitanguliza kuwalipa wakandarasi waliokuwa wamesimamisha kazi na kutoa malipo ya awali kwa miradi iliyosainiwa, kabla ya kuingia mikataba mipya ambayo ingeweza kuongeza madai ya riba.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amesema taratibu za manunuzi ya kipande cha takribani kilomita 42 kutoka Kibena hadi Kidegembye zimekamilika na mkandarasi amepatikana.
Kabla ya mkutano huo, Waziri Mkuu amezindua jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Njombe na kupanda mti wa parachichi katika eneo hilo.
Akitoa taarifa ya mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, William Mathew Makufwe, amesema ujenzi wa jengo umegharimu shilingi bilioni 3.8, huku shilingi milioni 300 zikitolewa kwa ajili ya samani.
Amesema jengo hilo linajumuisha ofisi za Mkurugenzi Mtendaji, Mwenyekiti wa Halmashauri na wakuu wa idara, pamoja na mifumo ya mawasiliano, usalama na huduma nyingine za kiutendaji.
