Na Victor Masangu,Kibaha

Halmashsuri ya Manispaa ya kibaha katika juhudi za kuongeza vyanzo vipya vya mapato yake ya ndani inatarajia kuweka na kuboresha huduma mbali mbali za kijamii katika mradi wa maegesho ya malori

Mradi huo wa maegesho ya malori ambao unatekelezwa katika eneo la Misugusugu utakuwa ni mkombozi mkubwa ya kuondokana na changamoto ya baadhi ya malori kupaki katika maeneo ya njiani.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Warda Maulid wakati akijibu maswali kutoka kwa baadhi ya madiwani wakati wa kikao cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha Julai- Septemba2026/2027.

Mkurugenzi huyo amebainisha kwamba kwa sasa wamejipanga kwa ajili ya kuweka huduma mbali mbali za kijamii katika eneo la mradi huo ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato kutokana na huduma zitakazotolewa.

“Nashukuru sana waheshimiwa kwa maswali na maoni yenu nimeyapokea na kwamba tutahakikisha tunaweka mipango ya muda mfupi na muda mredu katika eneo la mradi wetu wa maegesho katika eneo la misugusugu,”amebainisha Mkurugenzi.

Awali Diwani wa kata ya Misugusugu Ally Simba aliomba kwamba katika eneo hilo la maegesho linatakiwa kuboreshwa zaidi kwa kuweka pembezoni huduma mbali mbali za kijamii.

Naye Diwani wa viti maalumu Sara Uledi amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuyaondoa malori ambayo yamekuwa yakipaki njiani kiholela na kuyapeleka katika eneo maakumu ambalo limetengwa.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt Nicas amesema, baraza la madiwani linampongeza Mkurugenzi huyo kwa kuteuliwa na Mhe Rais, Dkt Samia Suluhu Hassani pia wanamkaribisha na kumuahidi ushirikiano wa hali na mali.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Fadhili Emanuel Nkurlu amewataka viongozi wa chama na serikali kuhakikisha kwamba kila mtu anatimiza wajibu wake ipasavyo kwa mujibu wa sheria na kanuni bila ya kuingiliana.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Mwl Mwajuma Amiri Nyamka amesema anapenda kuona uzalendo ushirikiano na mshikamano kutoka kwa Baraza la Madiwani ili kuweka ufanisi katika utendaji wa kazi.