Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa maelekezo kuhusu ukamilishaji wa miradi ya uboreshaji Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) Mkoa wa Mtwara, wakati alipotembelea mradi wa wajasiriamali unaojengwa Mtwara mjini, akiwa ziarani mkoani humo, leo tarehe 13 Novemba 2026.

……………

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, ameagiza TAKUKURU mkoani Mtwara kuchunguza mchakato wa utoaji wa tenda ya shilingi bilioni 27, namna mkandarasi alivyopatikana na walioidhinisha tenda hiyo, baada ya kutoridhishwa na kasi na kiwango cha utekelezaji wa miradi ya uboreshaji Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) Mkoa wa Mtwara, licha ya mkandarasi kulipwa TSh bilioni 4 za awali.

Tenda hiyo inahusisha ujenzi wa soko, barabara yenye urefu wa kilomita mbili, mtaro mkubwa wa maji na eneo la wajasiriamali.

Akijibu maswali ya Makamu wa Rais kuhusu mwenendo wa mradi, mshauri wa mradi kutoka Norplan (T) Ltd JV Typsa amesema tangu mwanzo mkandarasi kampuni ya Serengeti LTD alionyesha kutokuwa na uwezo wa kutekeleza kazi, huku akiwa na vifaa duni.

Mshauri huyo amekiri kuwa baadhi ya kazi hazijaanza kabisa na kwamba kiwango cha kazi zilizofanyika hakiendani na fedha zilizolipwa.

Makamu wa Rais amehoji pia sababu za mkandarasi kuwasilisha madai mengine ya malipo wakati kazi zilizotekelezwa haziendani na malipo ya awali.

Katika maelezo yaliyotolewa, mkandarasi ametajwa kuwa wa na vifaa vya daraja la saba, lakini amepewa kazi inayohitaji mkandarasi wa daraja la kwanza. Mkataba wake pia umeelezwa kukosa baadhi ya vifungu muhimu vya manunuzi ya serikali vinavyopaswa kumbana kutimiza wajibu wake.

Kufuatia hali hiyo, Makamu wa Rais ameagiza ujenzi wa miradi hiyo ukamilike ifikapo Machi Mosi, 2027, bila nyongeza ya muda. Ameelekeza kuwa mkandarasi akishindwa kukamilisha kazi kwa wakati, atozwe fidia ya ucheleweshaji (liquidated damages) na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.

Aidha, ametaka ujenzi wa mtaro wa maji upewe kipaumbele kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha. Ameagiza Waziri husika kupeleka taarifa kwa Waziri Mkuu ili afuatilie utekelezaji wa maelekezo hayo na kuhakikisha fidia inalipwa iwapo mkandarasi hatakamilisha kazi ndani ya muda uliowekwa.

Maagizo hayo yametolewa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara, akitembelea na kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kutatua kero za wananchi.