Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu akizungumza kwenye semina hiyo mkoani Arusha

…………
Na Happy Lazaro, Arusha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema Serikali inaandaa utaratibu mpya wa kisheria utakaoweka udhibiti katika uanzishwaji wa vyama vya wafanyakazi nchini, kufuatia ongezeko la vyama vinavyoanzishwa bila kuzingatia mifumo inayotakiwa.
Sangu amesema hali hiyo inaweza kudhoofisha ufanisi wa vyama vya wafanyakazi na kuvuruga namna vinavyotekeleza majukumu yake ya kuwatetea na kuwahudumia wanachama.
Akizungumza katika Semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE 2026, amesema Serikali inataka kuona vyama vilivyopo vikiboresha huduma na kuongeza tija kwa wanachama badala ya kuendelea kushuhudia ongezeko la vyama bila kuzingatia ubora wa huduma zake.
Amesema sheria inayotarajiwa kuletwa inalenga kuweka utaratibu katika sekta hiyo, huku ikilinda uhuru wa vyama vya wafanyakazi kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.
Sangu amewataka waajiri kuacha utaratibu wa kuwaingiza wafanyakazi wapya kwenye makato ya michango ya vyama vya wafanyakazi bila kuwashirikisha na kupata ridhaa zao.
Amesema baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakikatwa mishahara yao bila kuelewa kikamilifu umuhimu wa uanachama, hali inayoweza kuwanyima nafasi ya kufanya maamuzi kuhusu haki yao ya kujiunga na vyama hivyo.
Ameongeza kuwa, waajiri wana wajibu wa kuhakikisha wafanyakazi wanapata elimu ya kutosha kuhusu manufaa ya vyama vya wafanyakazi ili kila mmoja aweze kuamua kwa hiari yake kama anataka kuwa mwanachama au la.
“Hakuna mfanyakazi anayepaswa kulazimishwa kujiunga na chama chochote cha wafanyakazi, kwani uanachama ni suala la hiari na waajiri wanapaswa kuzingatia haki hiyo.”amesema Sangu.
Naye Katibu Mkuu wa TUGHE, Rugemalila Rutatina, amelalamikia baadhi ya waajiri wanaokwamisha uundaji wa mabaraza ya wafanyakazi na wengine kuingilia uhuru wa watumishi kwa kuwachagulia vyama vya kujiunga navyo watumishi wapya wanaoajiriwa na kuongeza kuwa hali hiyo inakwamisha haki za wafanyakazi kushiriki katika maamuzi yanayowahusu na kuchagua vyama vitakavyowawakilisha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu akizungumza kwenye semina hiyo mkoani Arusha
