Na Silivia Amandius
Bukoba.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo miradi inayotekelezwa kupitia mpango wa TACTIC, akieleza kutoridhishwa na kasi ya baadhi ya miradi licha ya kuwepo kwa fedha na wakandarasi.
Akizungumza katika baraza la madiwani la kikao Cha kwanza Cha robo ya mwaka wa fedha 2026/2027 amesisitiza umuhimu wa kusimamia kwa karibu ujenzi wa soko, barabara zinazolizunguka pamoja na mradi wa kingo za Mto Kanoni, akitaka miradi hiyo iende sambamba ili kukamilika kwa wakati na kurahisisha shughuli za wananchi na wafanyabiashara.
Aidha, ameitaka Halmashauri kuimarisha usimamizi wa ofisi za kata na mitaa, utatuzi wa migogoro ya ardhi na upangaji wa mji, huku akiwaonya viongozi wa mitaa wanaotumia madaraka yao vibaya katika masuala ya uuzaji wa maeneo.
Katika suala la usafi wa mazingira, Sima amesisitiza ushirikiano kati ya Halmashauri, kampuni za ukusanyaji taka na viongozi wa mitaa ili kuhakikisha maeneo yote yanapata huduma hiyo kwa kuzingatia mipango ya kila kata.
Pia ameitaka Halmashauri kuimarisha usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, akisisitiza umuhimu wa kuhakiki waombaji kwa kushirikisha madiwani na watendaji wa maeneo husika.
Akizungumzia huduma ya maji, ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) kupitia upya utaratibu wa uwekaji wa mita za maji ili kuondoa malalamiko ya wananchi wanaotozwa gharama za ziada za kuhamisha au kurejesha mita.
Vilevile, amewataka wazazi, walezi na viongozi wa maeneo husika kuongeza uangalizi kwa watoto wa kike kutokana na mwenendo wa baadhi ya wasichana wadogo kukutwa katika maeneo yasiyo salama nyakati za usiku, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kulinda usalama wao.
