▪ Azitaka taasisi kutekeleza maelekezo ya Rais kuhusu michezo mahali pa kazi

▪ Asisitiza uadilifu na ushiriki wa watu wenye ulemavu

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka wanamichezo kutumia ushawishi wao kuhimiza malezi bora kwa vijana na kuwa mfano katika kulinda maadili ya jamii.

“Wanamichezo mara zote ni watu wenye kauli kubwa. Ni watu wenye sauti inayosikika. Tuendelee kuwa sauti ya malezi kwenye nchi yetu,” amesema.

Dkt. Mwigulu ametoa wito huo leo (Alhamisi, Novemba 12, 2026), akimwakilisha Makamu wa Rais, Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi, katika ufunguzi wa mashindano ya 56 ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA), katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Amesema jamii haipaswi kufumbia macho mmomonyoko wa maadili kwa kudhani kuwa unawahusu watu au familia nyingine pekee, kwani athari zake zinaweza kuenea na kulikumba Taifa.

Amewataka wanamichezo kupaza sauti kuhimiza mambo mema, kama jamii ilivyoshirikiana kupambana na matumizi ya dawa za kulevya.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezitaka taasisi kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu kushirikiana na mashirikisho kama SHIMMUTA ili kuwawezesha wafanyakazi kushiriki michezo mahali pa kazi.

Amesisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kuyafanya sehemu ya maisha, badala ya kuyaona kama adhabu.

Kuhusu uendeshaji wa mashindano, Dkt. Mwigulu amewataka viongozi wa taasisi na timu kuhakikisha wanawasilisha majina ya washiriki wanaokidhi vigezo, ili ushindi unaopatikana uwe wa haki.

Pia, ameutaka uongozi wa SHIMMUTA kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika maandalizi na uhakiki wa washiriki, pamoja na kuweka mazingira yanayowezesha wanawake, wanaume na watu wenye ulemavu kushiriki kwa kuzingatia kanuni za michezo.

Amewataka wanamichezo kuheshimu waamuzi na washindani wao, kuzingatia kanuni na kuepuka vurugu, ubaguzi na udanganyifu.

“Timu yako ikifungwa mara hii, wewe omba uzima ije SHIMMUTA nyingine,” amesema, akisisitiza kuwa kushindwa kusiwe sababu ya kuvunja umoja na undugu.

Akizungumzia maandalizi ya AFCON 2027, Waziri Mkuu amewataka Watanzania, hususan watoa huduma, kuwa wakarimu kwa wageni na kutunza miundombinu ya michezo ili iendelee kutumika baada ya mashindano hayo.

Awali, Mwenyekiti wa SHIMMUTA, Marcel Bituro, amesema mashindano hayo yanalenga kuimarisha afya, mshikamano na tija mahali pa kazi. Pia, ameomba wadau kuunga mkono shirikisho hilo kupitia udhamini wa muda mrefu.