Na Mwandishi wetu

Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraka Leonard, amewataka Wabunge wa Bunge la Vijana 2026 kuzingatia misingi ya demokrasia, haki, nidhamu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao, huku wakiheshimu mitazamo tofauti na kuzingatia Kanuni na taratibu za Kibunge.

Ameyasema hayo leo, Novemba 10, 2026, wakati wa ufunguzi rasmi wa Bunge la Vijana 2026, lililoanza Novemba 9 na linatarajiwa kuhitimishwa Novemba 13, 2026, jijini Dodoma.

Amesema Bunge la Vijana ni jukwaa muhimu la kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora wa sasa na wa baadaye kwa kuwajengea uwezo wa kuelewa taratibu za Kibunge, misingi ya demokrasia, uongozi, uwakilishi na uwajibikaji.

Ameongeza kuwa mafunzo ya siku tano yanayotolewa kwa washiriki yamejikita katika maeneo mbalimbali, yakiwemo historia ya Bunge, uendeshaji wa shughuli za Kibunge, taratibu za kutunga na kupitisha sheria pamoja na Kanuni za Bunge la Vijana.

Aidha, ameeleza kuwa washiriki tayari wamefanya uchaguzi wa viongozi wa Bunge hilo, wakiwemo Spika, Naibu Spika na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Walio Wachache, pamoja na kupata Katibu wa Bunge na Makatibu Mezani watakaosaidia katika kuratibu na kusimamia shughuli za Bunge.

Vilevile, vijana hao wameshiriki katika mchakato wa kuthibitisha jina la Waziri Mkuu na uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hatua ambayo amesema imewapa uzoefu wa vitendo kuhusu mifumo ya kidemokrasia na taratibu za kiuongozi.

Akizungumza kuhusu wajibu wa viongozi waliochaguliwa, Katibu wa Bunge amewataka kuongoza kwa haki, usawa na busara, huku wakihakikisha kila Mbunge anapata nafasi ya kutoa maoni na kushiriki katika mijadala bila upendeleo.

Amewapongeza viongozi wote waliochaguliwa na kuwahimiza vijana ambao hawakupata nafasi za uongozi kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za Bunge kwa kutoa hoja, kujenga hoja mbadala na kuchangia mijadala yenye tija.

Amesisitiza kuwa uongozi si kushika nafasi pekee, bali ni dhamana inayopimwa kwa mchango, uwajibikaji na matokeo yanayopatikana kwa jamii inayowakilishwa.

“Uongozi si kushika nafasi pekee, bali ni kuwa na dhamira, uwezo na utayari wa kuleta mabadiliko. Bunge imara halijengwi na viongozi pekee, bali kwa ushiriki na michango ya kila Mbunge,” amesema Leonard.

Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kulitumia Bunge hilo kuibua na kujadili changamoto zinazowakabili wenzao katika maeneo mbalimbali, yakiwemo elimu, ajira, ujasiriamali, teknolojia, afya, mazingira, ushiriki katika maamuzi na fursa za kiuchumi.

Amewahimiza kutobainisha changamoto pekee, bali pia kuchambua chanzo chake na kutoa mapendekezo ya suluhisho yanayotekelezeka kwa manufaa ya vijana na Taifa kwa ujumla.

Katika hotuba yake, Pia amesisitiza mambo manne muhimu yatakayokuwa msingi wa mafanikio ya Bunge la Vijana 2026, ambayo ni nidhamu na uzingatiaji wa Kanuni za Bunge, uwezo wa kujenga hoja na kujadiliana kwa weledi, uwajibikaji katika kuwakilisha vijana pamoja na uadilifu, uzalendo na dhamira ya kulitumikia Taifa.

Amesema nidhamu ni msingi wa kuhakikisha mijadala inafanyika katika mazingira yenye heshima, utulivu na uvumilivu, huku akibainisha kuwa tofauti za kimawazo hazipaswi kuwa chanzo cha uhasama, bali ni fursa ya kupanua uelewa na kupata suluhisho bora zaidi.

Aidha, amewataka Wabunge wa Bunge la Vijana kujenga hoja kwa kuzingatia ukweli, ushahidi, mantiki na maslahi ya umma, akisisitiza kuwa uwezo wa kiongozi haupimwi kwa wingi wa maneno anayozungumza, bali kwa uwezo wa kusikiliza, kuchambua na kujibu hoja za wengine kwa busara.

Akizungumzia maadhimisho ya miaka 100 ya Bunge la Tanzania, Leonard amesema vijana hao watapata fursa ya kujadili na kupitisha Muswada wa Sheria unaohusu Maadhimisho ya Miaka 100 ya Bunge la Tanzania, jambo alilolieleza kuwa ni fursa ya kipekee kwao kushiriki katika hatua muhimu ya kihistoria ya Taasisi hiyo.

Amesema mwaka 2026 ni wa kihistoria kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo linaadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika, lililojulikana kama The Legislative Council of Tanganyika Territory, mwaka 1926.

Ameeleza kuwa maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kutafakari safari ya kihistoria ya Bunge, kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kuweka dira ya kuimarisha Taasisi hiyo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Miaka 100 ya Bunge: Historia Yetu, Dira Yetu,” inayosisitiza umuhimu wa kuhifadhi historia, nyaraka, uzoefu, misingi na tunu za Kibunge ili viendelee kuthaminiwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo.

Nae Spika wa Bunge la Vijana 2026, Anna Mrema, amewataka vijana kutambua kuwa wana wajibu wa kushiriki katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii na Taifa kwa kuanza kuchukua hatua sasa, badala ya kusubiri fursa za uongozi hapo baadaye au kulaumu viongozi kwa kushindwa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

 Aidha, amesisitiza umuhimu wa vijana kuzingatia nidhamu, uadilifu na heshima, akieleza kuwa uongozi ni dhamana na huduma kwa watu, si nafasi ya kujinufaisha binafsi. Ameongeza kuwa vijana walioshiriki Bunge hilo wanapaswa kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya watakaporejea katika vyuo na jamii zao, kwa kusambaza maarifa waliyoyapata na kuhamasisha wengine kushiriki katika shughuli za maendeleo.