Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa kampuni hiyo, Kisuma Mapunda akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo .
Wananchi wakipata maelezo kwenye banda hilo mara baada ya kutembelea katika maonesho hayo jijini Arusha
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .Kampuni ya mbolea ya Minjingu Mines and Fertilizer Limited imetambulisha aina mbalimbali za mbolea zinazolenga kuboresha afya ya udongo, kurejesha rutuba na kuongeza uzalishaji wa mazao kwa wakulima nchini.
Akizungumza katika maonesho ya Jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, linalofanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa kampuni hiyo, Kisuma Mapunda, amesema kampuni imeendelea kuzalisha mbolea zinazozingatia mahitaji ya wakulima na aina mbalimbali za mazao yanayolimwa nchini.
Mapunda amesema kampuni hiyo ina bidhaa tofauti zikiwemo Nafaka DAAP Plus yenye virutibisho vya msingi vya Naitrogeni (N), Fosiforasi (P) na Potasiamu (K) na virutubisho vya ziada vya Salfa, Kalsiamu, Magnisiamu, Zinki na Boron. Mbolea ya kukuzia ya CAAN Plus yenye virutubisho vya Naitrojeni, Fosiforasi na Kalsiamu.
Mapunda amesema mbolea hizo zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya mazao mbalimbali ili kuhakikisha wakulima wanapata virutubisho vinavyohitajika katika hatua tofauti za ukuaji wa mimea.
Amefafanua kuwa kwa wakulima wanaojihusisha na kilimo cha mboga mboga, kampuni inashauri matumizi ya Nafaka DAAP Plus wakati wa kupanda, ambayo ina virutubisho vinane vinavyosaidia ukuaji wa awali wa mimea.
Mapunda ameongeza kuwa, baada ya hatua ya kupanda, wakulima wanashauriwa kutumia CAAN Plus katika hatua ya kwanza ya kukuzia, mbolea ambayo ina virutubisho vitatu kwa ajili ya kusaidia ukuaji wa mimea.
Aidha, amesema katika hatua ya tatu ya ukuaji wa mboga mboga, wakulima wanaweza kutumia mbolea ya Pamba NPK ambayo imeandaliwa kusaidia kuongeza ufanisi wa uzalishaji wa mazao hayo.
“Utaratibu huo wa matumizi ya mbolea kulingana na hatua za ukuaji wa mimea unalenga kuwasaidia wakulima kupata matokeo bora na kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo.”amesema Mapunda.
Mapunda amefafanua kuwa tafiti za afya ya udongo nchini zimeonesha kuwepo kwa upungufu wa baadhi ya virutubisho katika maeneo mbalimbali, hali inayochangia kupungua kwa rutuba na kuathiri uzalishaji wa mazao.
Amesema kutokana na changamoto hiyo, kampuni imekuwa ikitengeneza mbolea zenye virutubisho vinavyolenga kukabiliana na upungufu huo, kurejesha rutuba ya udongo na kuboresha mazingira ya ukuaji wa mimea.
Akizungumzia uzalishaji wa mbolea hizo, amesema kampuni hiyo inachimba madini ya phosphate katika eneo la Minjingu, ambayo yana asili inayohusishwa na mabaki ya viumbe mbalimbali wakiwemo ndege aina ya flamingo, samaki na mimea.
Amefafanua kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikizingatia matumizi ya malighafi hizo katika kuzalisha mbolea zenye asili ya madini ya phosphate, huku ikilenga kulinda mazingira na kuboresha afya ya udongo kwa matumizi endelevu ya ardhi.
“Kampuni imeshirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) katika kuboresha baadhi ya bidhaa zake, ikiwemo mbolea ya Pamba NPK, kwa kuzingatia virutubisho vinavyohitajika kuongeza uzalishaji.”amesema Mapunda.
Aidha amesisitiza kuwa mbolea za Minjingu zimeandaliwa kwa kuzingatia tafiti na mazingira ya kilimo nchini, huku akiwahimiza wakulima kupata ushauri wa kitaalamu ili kutumia mbolea sahihi kwa mazao yao na kuongeza tija katika kilimo.
