Baadhi ya vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Bethelehemu Halmashauri ya Mji Mbinga Mkoani Ruvuma

………..

Na Mwandishi Maalum, Mbinga

WAZAZI wa kata ya Bethlehem Halmashauri ya Mji Mbinga Mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali kwa kujenga shule ya sekondari ya Bethlehem iliyowaondolea adha kwa watoto wao kutembea umbali mrefu kwenda kata nyingine kufuata masomo.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi wenzake Veronica Paul alisema,kukamilika kwa shule hiyo mpya kumewasaidia watoto wao kupunguza changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata shule,kupunguza gharama za usafiri kwa wazazi na mrundikano wa wanafunzi kwenye shule za jirani.

“Kwa kweli tulipoambiwa tunajengewa shule katika kata yetu tulifurahi sana ndiyo maana tulishirikiana na serikali kwa kusafisha eneo na kusaidia shughuli ndogo ndogo licha kazi kufanywa na mkandarasi ili shule ikamilike haraka”alisema.

Kapinga,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha na amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Mbina Amina Seif,kusimamia vizuri ujenzi wa shule hiyo ambayo imesaidia kupata elimu bora na ulinzi kwa watoto wao.

“Watoto wetu walikuwa wanapitia wakati mgumu sana kutoka sehemu moja kwenda nyingine kufuata shule,lakini sasa kupitia mradi huu tunamshukuru Rais Samia kwa kutambua changamoto ya shule katika kata yetu ya Bethlehem,awali tulikuwa na hofu juu ya usalama wa watoto barabarani”alisema.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo walisema,sasa wana uhakika wa kufikia malengo yao kwa sababu hakuna tena vikwazo vinavyoweza kuwasababishia washindwe kumaliza masomo kwani shule imejengwa karibu na maeneo wanayoishi na imewawezesha kupata muda mwingi wa kujisomea.

Shaina Abdul alisema, shule hiyo ina mazingira mazuri ya kujifunzia na kuwapunguzia gharama ya usafiri na kutumia muda mwingi barabarani kila siku kwenda shule nyingine zilizopo mbali na maeneo wanayoishi ili kufuata masomo.

Aidha alisema,shule hiyo imehamasisha wanafunzi wengi wa kata ya Bethlehem kupenda kwenda shule na kuongezeka kwa taaluma kwa sababu wanapata muda wa kujisomea ikilinganisha na awali ambapo walikuwa wanatumia muda mwingi barabarani kwenda na kurudi nyumbani.

Mwanafunzi mwingine Bosco Hyera alisema,shule hiyo itamsaidia kutimiza malengo yake kutokana na kuwa na miundombinu mizuri ya kujifunzia na kufundishia na walimu wenye ari kubwa ya kufanya kazi.

Mkuu wa shule hiyo Agnes Mapunda alisema,ujenzi wa shule hiyo ulianza mwaka 2024 na kukamilika mwaka 2025 ikiwa na wanafunzi 127 wavulana 53 na wasichana 83 ikiwa na vyumba vinane vya madarasa,maabara tatu,jengo la utawala,jengo la TEHAMA,maktaba matundu kumi ya vyoo na kichomea taka.

Mapunda,ameishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa Sh.milioni 560 kujenga shule hiyo ambayo imewasaidia wanafunzi wanaotoka katika kata ya Bethlehem na maeneo jirani kupata elimu karibu na maeneo yao,hivyo kumaliza kero ya kutembea umbali mrefu kwenda kata nyingine kufuata masomo.

Amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Mbinga Amina Seif, kwa kusimamia ujenzi wa mradi huo na kuongeza kiasi cha Sh.milioni 177 kutoka mapato ya ndani zilizotumika kukamilisha ujenzi wa shule hiyo .

“Nawashukuru wenyeji wa eneo hili kwa kukubali kutoa ardhi yao na kushiriki kwa karibu ujenzi wa shule hii,kwa sababu wangekataa leo shule isingekuwepo kwani ukiangalia unaona shule imezungukwa na makazi ya watu”alisema Mwalimu Mapunda.

Ametoa wito kwa wanafunzi,kutumia fursa ya kuletewa shule jirani kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na wazazi kuleta watoto wao kusoma na kufuatilia maendeleo yao badala ya kuwaachia walimu na Serikali.