Na Mwandishi wa OTR
Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeahidi kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) katika kuharakisha mageuzi yanayolenga kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi wa mashirika ya umma nchini.
Ahadi hiyo ilitolewa Jumamosi, Novemba 7, 2026, na Mwenyekiti wa PIC, Mhe. Ojambi Masaburi, wakati wa ziara ya kamati hiyo katika OTR jijini Dar es Salaam, akisisitiza umuhimu wa taasisi hizo kufanya kazi kwa karibu ili kutimiza maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha utendaji wa taasisi za umma.
Mhe. Masaburi alisema PIC iko tayari kutoa ushirikiano na kuitetea OTR pale inapohitaji msaada wa kamati hiyo, akieleza kuwa mafanikio ya mageuzi yanahitaji mshikamano na utayari wa pande zote kutimiza wajibu wao.
“Uwezo wa kuwasaidia tunao na nia hiyo tunayo,” alisema, akihimiza pande hizo kuendelea kufanya kazi kama familia ili kufanikisha malengo yaliyowekwa na Mhe. Rais.
Katika ziara hiyo, wajumbe wa PIC walipokelewa na Menejimenti na viongozi wengine waandamizi wa OTR wakiongozwa na Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu.
Kwa upande wake, Bw. Mchechu aliishukuru kamati hiyo kwa ziara yake na ushirikiano ambao imekuwa ikiipatia OTR, akiahidi kuendeleza uhusiano huo kwa manufaa ya taasisi za umma na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Alisema safari ya mageuzi katika mashirika ya umma inaendelea vizuri, huku akibainisha kuwa bado kuna maeneo yanayohitaji maboresho ili taasisi hizo ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Kwa mujibu wa Bw. Mchechu, kati ya asilimia 70 na 90 ya wakuu wa taasisi tayari wanafahamu wajibu wao na kile kinachotarajiwa kutoka kwao, jambo alilolitaja kuwa hatua muhimu katika safari ya mageuzi.
“Asilimia 70 hadi 90 ya wakuu wa taasisi wanajua nini wanapaswa kufanya. Hii ni hatua kubwa katika safari ya mageuzi ya mashirika ya umma,” alisema.
Hata hivyo, Bw. Mchechu alisema hatua inayofuata katika safari hiyo ni kuhakikisha uelewa wa majukumu unaambatana na uwezo wa kuyatekeleza kwa vitendo.
Alieleza kuwa msisitizo wa OTR kwa sasa ni kuona wakuu wa taasisi wanachukua hatua zinazohitajika, wanafanya maamuzi sahihi na kuhakikisha majukumu ya taasisi zao yanatekelezwa kwa ufanisi.
Kauli hiyo inaweka msisitizo katika hatua inayofuata ya mageuzi, ambayo ni kugeuza uelewa wa majukumu kuwa utekelezaji wenye matokeo yanayopimika, uwajibikaji na utendaji bora wa mashirika ya umma.

