Na Mwandishi Wetu , Dar es Salaam
Wadau Madale Saccos iko katika hatua za mwisho za usajili, huku wanachama 138 kati ya wanachama 334 wa Umoja wa Wadau Madale wakiwa wamejiunga na ushirika huo unaotarajiwa kuanza rasmi shughuli zake baada ya kukamilika kwa taratibu za usajili na uchaguzi wa viongozi.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka uliofanyika jana katika ukumbi wa Madale Flamingo, Mgeni Rasmi, Zahra Kamtande kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Manispaa ya Kinondoni, alisema zoezi la usajili limefikia takribani asilimia 90 na kwamba nyaraka za chama hicho zimekamilika kwa sehemu kubwa.
Alisema hatua iliyobaki ni kukamilisha taarifa za wanachama katika mfumo wa usajili, ikiwemo majina, namba za NIDA, tarehe za kuzaliwa, idadi ya hisa na namba za simu, ili kupata namba ya malipo na kuendelea na taratibu za uchaguzi wa viongozi.
Kamtande alisema mfumo huo umeanzishwa ili kuhakikisha usajili wa vyama vya ushirika unakuwa wa uhakika na kuondoa uwepo wa vyama visivyo na uhalisia wa wanachama, akiwataka wanachama kuendelea kuwa na uvumilivu wakati taratibu hizo zikikamilishwa.
Aliwapongeza viongozi na wanachama wa Wadau Madale kwa hatua waliyoifikia, akisema mafanikio ya vyama vya ushirika yanatokana na mshikamano, uzalendo na dhamira ya wanachama kukiendeleza chama chao.
Alitoa mfano wa chama cha ushirika cha Tegeta Friendship kilichopo Ununio, ambacho alisema kimepiga hatua kubwa na kufikia uwezo wa kutoa mikopo hadi Sh milioni 50 kwa wanachama wake, akisema mafanikio hayo yanatokana na kujituma na mshikamano wa wanachama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wadau Madale, Stephen Kazimoto, alisema kukamilika kwa usajili kutatoa nafasi kwa chama kuanza rasmi shughuli zake, ikiwemo uchaguzi wa viongozi watakaosimamia maendeleo ya ushirika huo.
Kazimoto alisema wanachama 334 wa umoja huo ni tofauti na wanachama 138 waliojiunga na Saccos, akifafanua kuwa wale ambao hawajakamilisha taratibu za kujiunga watakapofanya hivyo baadaye wataingia kwa utaratibu wa wanachama wapya.
Alionya kuwa baada ya usajili kukamilika, masharti ya kujiunga na Saccos yanaweza kubadilika kulingana na miongozo itakayowekwa na viongozi watakaochaguliwa, ikiwemo kiwango cha kiingilio, hivyo akawahimiza wenye nia ya kujiunga kufanya hivyo mapema.
Kazimoto alisema viongozi wa Saccos wanatarajiwa kupatikana ndani ya mwezi Novemba mwaka huu ili ushirika huo uzinduliwe na kuanza kutoa huduma kwa wanachama wake.
Naye Katibu wa Wadau Madale, Issa Mnasha, akiwasilisha muhtasari wa mkutano mkuu wa mwaka 2025, alisema umoja huo umeendelea kupokea wanachama wapya na kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii, huku kamati za uongozi zikiendelea kusimamia masuala ya umoja, maadili na ustawi wa wanachama.
Mnasha alisema mkutano mkuu wa mwaka 2025 uliridhia kuongeza kiingilio cha wanachama wa umoja kutoka Sh 200,000 hadi Sh 500,000, pamoja na kuweka ukomo wa wanachama 350.
Alisema pia mkutano huo uliridhia matumizi ya Sh 150,000 kwa vikao vya Kamati Kuu na Kamati Tendaji, huku kamati ya maadili na usuluhishi ikisisitiza umuhimu wa wanachama kuheshimiana, kudumisha upendo na kuimarisha umoja.
Mkutano huo pia ulipokea na kujadili taarifa mbalimbali za kamati tendaji, fedha, uongozi, maadili na nidhamu pamoja na burudani na masuala ya kijamii, ukiwa sehemu ya maandalizi ya kuimarisha ushirika wa Wadau Madale katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa Saccos.

