Uelewa wa sheria za usalama barabarani miongoni mwa wanafunzi ni sehemu muhimu ya kupunguza ajali na kujenga jamii inayozingatia matumizi sahihi ya barabara, huku Shule ya Sekondari Itega ya jijini Dodoma ikiibuka mshindi wa mashindano ya usalama barabarani yaliyoandaliwa kwa udhamini wa kampuni ya TotalEnergies marketing tanzania.

Itega imewashinda washindani wake, Shule za Sekondari Wella na Dodoma, na kujinyakulia zawadi ya shilingi milioni 15 zitakazotumika kuboresha mazingira ya usalama barabarani katika shule hiyo.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi hizo, Afisa Taaluma wa Mkoa wa Dodoma, Mwalimu Justin Machela, amewataka wanafunzi walioshiriki mashindano hayo kutumia elimu waliyoipata kuwaelimisha wengine kuhusu umuhimu wa kufuata sheria za barabarani.

Amesisitiza kuwa wanafunzi wanapaswa kuwa mfano katika matumizi sahihi ya barabara, kutoa taarifa kuhusu maeneo hatarishi kwa walimu na mamlaka husika, pamoja na kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuimarisha usalama bila kujiweka katika mazingira ya hatari.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria wa TotalEnergies Marketing Tanzania Limited, Marsha Msuya, amesema tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2022, kampuni hiyo imetumia zaidi ya shilingi milioni 400 katika kuratibu programu hiyo nchini.

Amesema mashindano hayo yanakwenda zaidi ya ushindani wa shule, kwani wanafunzi hupewa mafunzo ya usalama barabarani na kutakiwa kuchunguza mazingira ya shule zao ili kubaini changamoto na kubuni hatua za kupunguza vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali.

Naye Sajenti Ester Makali kutoka Dawati la Elimu kwa Umma la Kikosi cha Usalama Barabarani amesisitiza umuhimu wa elimu hiyo kuwafikia wanafunzi na jamii kwa ujumla, huku Nancy Augustino Mathias, balozi wa usalama barabarani kutoka Itega, akieleza dhamira ya wanafunzi kutumia uelewa walioupata kuhamasisha wengine.

Baada ya ushindi huo, Itega inatarajiwa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kikanda yatakayoshirikisha nchi mbalimbali zikiwemo Uganda, Madagascar na Ivory Coast, kabla ya kupatikana kwa mshindi atakayekwenda kushiriki mashindano ya dunia.