Ukosefu wa ajira, ugumu wa maisha na changamoto za upatikanaji wa fursa za kiuchumi ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuchochea mwamko wa vijana kutaka mabadiliko ya kikatiba nchini Tanzania.

Hayo yameelezwa leo Novemba 7,2026 jijini Dodoma na Meneja wa uchechemuzi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Raymond Kanegene wakati wa mafunzo ya Kanzidata ya Katiba (Katiba Database) kwa wanafunzi na kuongeza kuwa sehemu ya pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza misingi ya haki za msingi, ikiwemo haki ya elimu na kazi, lakini inaweka mipaka katika namna haki hizo zinavyoweza kudaiwa mahakamani.

“Hali hiyo inaibua umuhimu wa wananchi hususani vijana, kuelewa Katiba na kushiriki katika mchakato wa kutoa maoni ili kupendekeza marekebisho yatakayowezesha haki zinazotajwa katika Katiba kulindwa na kudaiwa kwa njia za kisheria,”amesema.

Ameeleza kuwa wito huo haupaswi kuchukuliwa kama sababu ya kuingia katika vurugu, bali ni fursa ya kutumia njia za kikatiba na kisheria katika kutafuta mabadiliko.

Katika kueleza mwitikio wa wananchi kuhusu kampeni hiyo, amesema tangu kuzinduliwa kwake Septemba 15, 2026, kumekuwa na mwamko wa kufuatilia mijadala ya Katiba hususani kupitia video ambazo zimeripotiwa kufikiwa na zaidi ya watu laki moja, huku wengine wakitumia vitabu na magazeti kupata elimu hiyo.

“Vijana ni miongoni mwa makundi yanayoonyesha shauku ya kutaka haki, wakihusisha mahitaji ya Katiba na hali halisi ya maisha yao ikiwemo ukosefu wa ajira kwa wahitimu, ugumu wa kupata fursa za kiuchumi na malalamiko kuhusu upendeleo katika ajira,”amesema.

Hata hivyo, changamoto iliyopo ni kuhakikisha kuwa vijana hawabaki kuwa watazamaji wa mijadala hiyo, bali wanatumia nafasi zilizopo kutoa maoni na kushiriki katika kujenga mfumo wa kikatiba unaowezesha haki kutambuliwa, kulindwa na kutekelezwa.