Muasisi wa Taasisi ya UKORC Foundation Tanzania, Kheri Shida akizungumza jijini Arusha.

……………
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .Muasisi wa Taasisi ya UKORC Foundation Tanzania, Kheri Shida, amesema taasisi hiyo inatarajia kuanzisha kituo cha tiba na marekebisho ya tabia kwa waraibu wa dawa za kulevya katika Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza uraibu na uhalifu unaohusishwa na matumizi ya dawa hizo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha , Kheri amesema tayari taasisi hiyo imepata eneo lenye ukubwa wa ekari 57 wilayani Pangani kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, huku akieleza kuwa mwaka 2027 wanatarajia kuanza na huduma za awali kupitia kituo maalumu cha kupokea na kuwahudumia waraibu (Drop-in Centre).
Amesema wazo la kuanzisha taasisi hiyo limetokana na uzoefu alioupata nchini Italia ambako amefanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 katika huduma za kijamii, hususani kusaidia watu walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya kupitia mfumo wa kuwapatia tiba badala ya kuwafunga gerezani.
Kheri ameeleza kuwa mfumo huo unaojulikana kama Deflection unalenga kuwapa watu waliojihusisha na makosa madogo yanayohusiana na uraibu nafasi ya kupata matibabu na kurekebisha maisha yao katika vituo maalumu badala ya kupelekwa gerezani, ambako kwa mtazamo wake wanaweza kukutana na mazingira yanayochochea uhalifu zaidi.
Kheri amefafanua kuwa, UKORC Foundation imekuwa ikishirikiana na Jeshi la Polisi, hususani Polisi Jamii na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), pamoja na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi ili kujenga mfumo wa ushirikiano utakaowezesha waraibu kupata huduma za matibabu na kurejea katika jamii wakiwa wameimarika.
“Ushirikiano huo unaweza pia kusaidia kupunguza mzigo kwa vyombo vya dola kwa kuwa baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu, ikiwemo wizi na biashara ndogo za dawa za kulevya, hufanya hivyo ili kupata fedha za kuendeleza matumizi yao kutokana na gharama za kupata dawa hizo.”amesema Kheri.
Aidha, amesema mpango huo unahusisha pia huduma za matibabu ikiwemo Methadone kwa watu wanaostahili, ambayo husaidia kudhibiti utegemezi wa dawa za kulevya na kuwawezesha waraibu kuanza safari ya kupona, hatua inayoweza kuchangia kupunguza vitendo vya uhalifu vinavyohusishwa na uraibu.
“”Kuhusu ushirikiano wa taasisi mbalimbali, Kheri amesema tayari wamekuwa wakifanya mikutano na wadau wakiwemo polisi na majaji katika maeneo mbalimbali kama Dodoma na Arusha, kwa lengo la kuunganisha mahakama, polisi na vituo vya tiba ili kuhakikisha mfumo wa kuwaelekeza waraibu kwenye huduma za matibabu unatekelezwa kwa ufanisi.”amesema Kheri.
Amesema kwa mujibu wa maelezo aliyoyapata kutoka kwa wadau wa DCI, Tanzania ina sheria zinazotoa nafasi ya kushughulikia baadhi ya watu wanaofanya makosa madogo kwa kuwaelekeza kwenye vituo mbadala vya matibabu badala ya kuwapeleka gerezani, hivyo uwepo wa kituo cha UKORC Foundation utasaidia kutoa huduma zinazohitajika katika utekelezaji wa mfumo huo.
Aidha ametoa wito kwa jamii kuacha kuwanyanyapaa watu walioathirika na dawa za kulevya kwa kuwa wanaweza kupata matibabu, kubadilika na kurejea katika maisha ya kawaida, akisisitiza kuwa kaulimbiu ya taasisi hiyo ni “We Stand for Recovery, Not Stigma”, akimaanisha kuwa wanasimamia uponyaji badala ya unyanyapaa.
