NA DENIS MLOWE, IRINGA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa imesaidia kusimamia urejeshaji wa Sh381.8 milioni zilizokuwa zinadaiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutoka kwa waajiri waliokuwa hawawasilishi michango ya wafanyakazi wao, hatua inayolenga kulinda haki na maslahi ya wanachama wa mfuko huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Victor Swella,, Kaimu Meneja wa TAKUKURU mkoa Janeth Haule alisema kuwa
hatua hiyo ni sehemu ya mafanikio ya utendaji wa taasisi hiyo ikilenga kuhakikisha waajiri wanatimiza wajibu wao wa kisheria wa kuwasilisha michango ya wafanyakazi katika NSSF.
Alisema kuwa atika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, TAKUKURU ilifanikiwa kusimamia marejesho ya Sh381,829,981 baada ya kufanya uchambuzi wa mifumo ya uzingatiaji wa Sheria ya Hifadhi ya Jamii na kubaini waajiri waliokuwa na madeni ya michango ya watumishi wao.
Alisema NSSF ina jukumu la kukusanya michango ya hifadhi ya jamii kutoka kwa waajiri na wafanyakazi na kuhakikisha wanachama wanapata mafao yao wanapostahili, hivyo kutowasilishwa kwa michango hiyo kunaweza kuathiri haki za wafanyakazi.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU Mkoa wa Iringa ilipokea malalamiko 68 katika kipindi hicho, ambapo malalamiko tisa yalihusu vitendo vya rushwa. kati ya hayo, sita yalihamishiwa katika mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi.
Aidha, taasisi hiyo ilifungua kesi mpya nane mahakamani, huku kesi saba zikimalizika kwa ushindi wa Jamhuri na kesi 14 zikiendelea kusikilizwa mahakamani.
Akizungumzia mikakati ya robo ya pili ya mwaka 2026 alisema TAKUKURU itaendelea kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika sekta za kipaumbele ikiwemo maji, afya na barabara, pamoja na kuchunguza ushirikishwaji wa wananchi katika mikutano na vikao vya maamuzi vya Serikali za Mitaa.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo itaendelea kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi ya Jamii, kushughulikia kero za wananchi kupitia programu ya TAKUKURU Rafiki na kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu madhara ya rushwa.
Haule aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushiriki wa kila mmoja.
Alisisitiza kuwa ushirikiano, uwajibikaji na uzalendo ni nguzo muhimu katika kuhakikisha vitendo vya rushwa vinatokomezwa katika jamii.
Kaulimbiu ya TAKUKURU katika mapambano hayo ni: “Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu.”
