Na Mwandishi Wetu – GENEVA, Uswisi
Leo, Novemba 6, 2026, Tanzania inatarajiwa kuwasilisha mafanikio, mageuzi na hatua zilizotekelezwa katika kuimarisha utawala wa sheria, upatikanaji wa haki na ustawi wa wananchi katika Mapitio ya Nne ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR) ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika Kikao cha 53 cha Kikundi Kazi cha UPR kinachoendelea jijini Geneva kuanzia Novemba 2 hadi 13, 2026.
Ushiriki huo unaipa Tanzania fursa ya kuieleza Jumuiya ya Kimataifa utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa katika mapitio yaliyopita, hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita na maeneo yanayoendelea kupewa kipaumbele katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na utekelezaji wa haki za binadamu nchini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Novemba 04, 2026 jijini Geneva, Uswiswi kuhusu ushiriki wa Tanzania katika mapitio hayo, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Ulega, amesema chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia falsafa ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya (4Rs), Serikali inaendelea kuimarisha diplomasia, utawala bora na ulinzi wa haki za binadamu
“Tanzania inashiriki katika duru ya nne ya UPR ikiwa tayari imeshiriki katika mapitio matatu yaliyotangulia mwaka 2011, 2016 na 2021. Mapitio yatakayofanyika sasa, ni fursa muhimu kwa Tanzania kueleza mafanikio yaliyopatikana, hatua zilizochukuliwa kutekeleza mapendekezo yaliyokubaliwa katika duru zilizopita, pamoja na kuonesha dhamira ya kuendelea kuimarisha haki za binadamu na ustawi wa wananchi”, amesema Mhe. Ulega.
Waziri Ulega ameongeza kuwa, tangu mapitio ya mwaka 2021, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika maeneo yanayogusa ustawi wa wananchi, yakiwemo utawala wa sheria, upatikanaji wa haki, afya, elimu, upatikanaji wa maji na miundombinu ambapo hatua hizo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mazingira ya haki, usawa wa fursa na maendeleo jumuishi.
Amefafanua kuwa, taarifa hiyo inaainisha mafanikio, mageuzi na hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2026, ikieleza juhudi za kuimarisha mifumo ya haki za binadamu kama msingi wa maendeleo endelevu ambapo ushiriki wa Tanzania katika mapitio hayo unaendana pia na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga taifa lenye ustawi, haki, ujumuishi na uwezo wa kujitegemea.
Vile vile ameeleza kuwa, maandalizi ya taarifa hiyo yamehusisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikisha Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Mahakama, Asasi za Kiraia, taasisi za kidini, mashirika ya watu wenye ulemavu na wadau wengine wa haki za binadamu.
UPR ni utaratibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa unaozipa nchi zote wanachama fursa ya kupitia hali ya haki za binadamu katika nchi zao kwa misingi ya usawa. Kupitia utaratibu huo, nchi huwasilisha taarifa kuhusu hatua zilizochukuliwa, mafanikio na changamoto zilizopo, huku mataifa mengine yakitoa mapendekezo yanayolenga kuimarisha zaidi utekelezaji wa haki za binadamu.

