HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imetoa Shilingi milioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Kata ya Viziwaziwa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa kituo cha polisi katika eneo hilo.

Ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka 2023 kwa nguvu za wananchi pamoja na wadau wa maendeleo, huku gharama za mradi huo zikikadiriwa kufikia zaidi ya Shilingi milioni 260.Akizungumza wakati wa kufungua rasmi ujenzi wa kituo hicho sambamba na harambee ya kuchangisha fedha na vifaa vya ujenzi, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, amewapongeza wananchi kwa kuanzisha mradi huo na kuonesha mshikamano katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Dkt. Mawazo amesema Halmashauri itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo, huku akieleza matarajio yake kuwa kituo hicho kitakuwa kimekamilika ifikapo Julai 2027.

Aidha, amechangia mabati 500 kwa ajili ya kuezeka jengo hilo ili kuwezesha kuanza kutumika na kutoa huduma kwa wananchi.

Amesema wananchi wamechangia takribani Shilingi milioni 12 tangu kuanza kwa mradi huo na kwamba hatua hiyo inaonesha namna jamii inavyoweza kuibua na kuanzisha miradi ya maendeleo, huku Serikali ikiingia kusaidia kuikamilisha.

Naye Diwani wa Kata ya Viziwaziwa, Mohamed Chamba, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuleta fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na Mstahiki Meya kwa mchango wake wa mabati 500.

Pia amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Kibaha, Silvestry Koka, huku akiwahimiza wadau wa maendeleo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ili kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho unakamilika.

Katika harambee hiyo, madiwani wa Kata za Misugusugu na Visiga, Ally Mwinyi Simba na Saidi Mpaki, wameshiriki na kuahidi kushirikiana kuhamasisha wadau wa maendeleo kuchangia ili kituo hicho kikamilike ndani ya muda uliopangwa.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kata ya Viziwaziwa wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema kukamilika kwa kituo hicho kutamaliza kero ya muda mrefu ya ukosefu wa huduma za polisi katika eneo lao.

Wananchi hao pia wamempongeza Mstahiki Meya kwa kuendesha harambee iliyowezesha kupatikana kwa Shilingi 900,000, tofali 750 na mifuko 10 ya saruji kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo hicho.