Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum akipokea folder lenye taarifa za huduma zinazotolewa na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kutoka kwa Daktari Bingwa na Mbobezi wa Magonjwa ya Saratani wa Taasisi hiyo, Caroline Swai alipotembelea banda la ORCI wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake wa Jukwaa la Mabunge la Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) uliomalizika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
……
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
05/11/2026 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum amewataka wananchi kujenga utaratibu wa kufanya uchunguzi wa afya zao angalau mara moja kwa mwaka ikiwemo uchunguzi wa saratani ili kubaini magonjwa mapema na kupata matibabu kwa wakati.
Dkt. Saada ametoa wito huo leo alipotembelea banda la Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) lililokuwepo kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake wa Jukwaa la Mabunge la Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) uliomalizika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Alisema mtindo usiofaa wa maisha, ikiwemo ulaji usiozingatia kanuni za lishe bora, kutofanya mazoezi, matumizi ya bidhaa za tumbaku na unywaji wa pombe kupita kiasi ni miongoni mwa mambo yanayoweza kusababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza hivyo ni basi muhimu kwa wananchi kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kufahamu hali zao za kiafya.
Aliongeza kuwa watu wengi hupoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo saratani kwa sababu ya kuchelewa kugundulika kwa magonjwa hayo na kusisitiza kuwa uchunguzi wa mapema husaidia kubaini tatizo na kuwezesha mgonjwa kupata matibabu kwa wakati.
“Tunaishukuru Serikali yetu imewekeza vya kutosha katika sekta ya afya kwa kusomesha wataalamu na kuwa na vifaa tiba vya kisasa na vya kutosha. Ndiyo maana sasa hivi Taasisi yetu ya Saratani Ocean Road inatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa ya saratani kwa Watanzania na wasio Watanzania,” alisema.
Dkt. Saada alisema ORCI imeonesha jitihada za kuwafikia wananchi kwa kutoa huduma za uchunguzi wa awali na elimu kuhusu saratani katika maeneo mbalimbali.
“Ninawapongeza ORCI kwa kutoa huduma za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya saratani pamoja na kutoa elimu katika mkutano huu na maeneo mengine. Nawaomba muendelee kutoa huduma hiyo ili wananchi wengi zaidi wawe na uelewa kuhusu magonjwa haya,” alisema.
Akizungumzia huduma zilizotolewa na ORCI katika mkutano huo Daktari Bingwa na Mbobezi wa Magonjwa ya Saratani wa Taasisi hiyo, Caroline Swai alisema jumla ya washiriki 81 walipata huduma za uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti na saratani ya mlango wa kizazi pamoja na elimu ya magonjwa hayo ambapo 12 kati yao walitoka nje ya Tanzania.
Alisema ushiriki wa ORCI katika mkutano huo ulilenga kuitangaza Taasisi na huduma zake, kutoa elimu kuhusu saratani pamoja na kusogeza huduma za uchunguzi wa awali karibu na washiriki ambao wengi wao walikuwa wanawake.
“Washiriki wengi wa mkutano huu ni wanawake, hivyo tumeona ni muhimu kuwaletea huduma za uchunguzi wa saratani zinazowakabili zaidi wanawake katika ukanda huu wa Afrika zikiwemo saratani ya matiti na saratani ya mlango wa kizazi,” alieleza Dkt. Caroline.
Dkt. Caroline alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa za uchunguzi na matibabu ya saratani, hatua inayoiwezesha ORCI kuimarisha utoaji wa huduma za kibingwa kwa kutumia vifaa tiba vya kisasa.
Alitaja uwepo wa mashine ya PET-CT Scan kuwa miongoni mwa mafanikio ya uwekezaji huo akieleza huku akieleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache katika ukanda wa Kusini mwa Afrika zenye teknolojia hiyo pamoja na Afrika Kusini.
Dkt. Caroline alisema baadhi ya washiriki waliotembelea banda la ORCI walivutiwa na elimu na taarifa walizopata kuhusu huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo, huku baadhi ya washiriki kutoka nje ya nchi wakionesha nia ya kuleta wagonjwa wao kupata matibabu nchini Tanzania.
Kwa upande wake Afisa Muuguzi wa ORCI, Dativa Mushi aliyekuwa akitoa huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti katika mkutano huo alieleza kuwa miongoni mwa dalili zinazoweza kuashiria saratani ya matiti ni uvimbe kwenye titi ambao unaweza kuwa mgumu na usio na maumivu.
Alizitaja dalili nyingine kuwa ni pamoja na kubadilika kwa ukubwa au umbo la titi, chuchu kuvutika ndani, ngozi ya titi kuwa nyekundu au kupata mikunjo inayofanana na ganda la chungwa, vidonda kwenye chuchu au titi visivyopona, pamoja na uvimbe kwenye kwapa unaoweza kusababishwa na kuvimba kwa tezi za limfu.
Nao washiriki waliopata huduma za uchunguzi wa saratani waliishukuru ORCI kwa kuwapatia fursa ya kufahamu hali zao za kiafya na kupata elimu kuhusu umuhimu wa kujikinga na saratani kupitia uchunguzi wa mapema.
“Ninaipongeza ORCI kwa kutumia fursa ya mkutano huu kuwafikia wanawake kwa kutoa elimu na huduma za uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi. Nimefika hapa kujionea namna wanavyowahudumia wabunge wanawake kwa kuwapatia fursa ya kupima na kufahamu hali za afya zao, nami nikaona nitumie nafasi hii kupima afya yangu,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Christine Mwakatobe.
“Katika mkutano huu nimetembelea banda la Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kwa ajili ya kupata elimu ya magonjwa ya saratani, hususan saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti ambapo pia nimepata fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani hizo,” alisema Given Matumba ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) imeendelea kutoa huduma za elimu na uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti na saratani ya mlango wa kizazi kwa washiriki wa mikutano na makundi mbalimbali ya jamii ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uelewa kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa mapema na kuwahamasisha wananchi kuchukua hatua za kulinda afya zao.
