Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amezitaka nchi wanachama wa Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) kutekeleza kwa vitendo makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa wanawake wabunge kuhusu amani, usalama na maendeleo, akisisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano wa kikanda.
Akizungumza leo Novemba 5,2026 wakati wa kufunga mkutano wa wanawake wabunge wa Jukwaa la Mabunge la ICGLR uliofanyika Dar es Salaam kuanzia Novemba 2 hadi 5, 2026, Zungu amesema mafanikio ya mkutano huo yatapimwa kwa hatua zitakazochukuliwa na nchi wanachama kutekeleza maazimio yaliyopitishwa.
Amesema Tanzania inathamini ushiriki wa wajumbe wote na mchango wa wadau mbalimbali waliofanikisha mkutano huo, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake unaoendelea kuiweka Tanzania katika nafasi ya kuhimiza amani, mazungumzo, ushirikiano wa kikanda na maendeleo jumuishi.
Zungu pia amemshukuru Makamu wa Rais,Deogratius Ndejembi aliyemwakilisha Rais Samia katika ufunguzi wa mkutano huo, akisema Serikali imeonesha dhamira ya kuimarisha ushiriki wa wanawake katika michakato ya amani na usalama kupitia Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Wanawake, Amani na Usalama wa mwaka 2025–2029.
Kwa upande wake, Katibu mkuu(ICGLR) barozi Dk. Deo Mwapinga, amesema matokeo ya mkutano huo yanapaswa kufuatiwa na hatua za utekelezaji pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa uratibu na ufuatiliaji wa maendeleo ya maazimio yaliyokubaliwa.
Mwapinga amesema mfumo huo utasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama, kufuatilia utekelezaji na kuhakikisha Mpango wa Kikanda wa Wanawake, Amani na Usalama wa mwaka 2027–2031 unatekelezwa kwa ufanisi na uratibu unaofaa.
Amesema mkutano huo umepitisha Azimio la Dar es Salaam linalozitaka nchi wanachama kuimarisha sheria na mifumo ya kitaasisi inayowezesha wanawake kupata uwakilishi sawa katika mabunge, serikali na nafasi za uongozi wa vyama vya siasa.
Amesema azimio hilo pia linahimiza kuongezwa kwa ushiriki wa wanawake katika majadiliano ya amani na timu za upatanishi, kuzuia ukatili dhidi ya wanawake katika siasa, pamoja na kuhakikisha wanaoshiriki katika michakato ya amani wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mwapinga amesema wajumbe wamekubaliana pia kuimarisha usimamizi wa rasilimali za asili kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, kupambana na unyonyaji haramu wa rasilimali unaochochea migogoro na kuhakikisha wanawake wanapata sehemu stahiki ya manufaa yatokanayo na rasilimali hizo.
Aidha, amesema azimio hilo limeweka msisitizo katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia upatikanaji wa mikopo, ardhi, masoko, biashara za mipakani na elimu ya fedha na teknolojia, huku likitaka kulindwa kwa wanawake na wasichana wakimbizi na waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na migogoro na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema azimio hilo limeitaka Sekretarieti ya ICGLR kufuatilia utekelezaji wake na kuwasilisha taarifa katika kikao kijacho cha kawaida cha Bunge la Umoja huo, huku likihimiza viongozi wa kikanda kulifikisha kwa wakuu wa nchi na serikali, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.
Naye, waziri wa maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto Serikali ya mapinduzi Zanzibar Saada Mkuya, amesema Serikali inaichukulia ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama kuwa sehemu muhimu ya malengo mapana ya maendeleo ya Taifa, kwa kuwa uwezeshaji wa wanawake ni msingi wa kujenga familia imara na jamii zenye ustahimilivu.
Dkt.Mkuya amesema dhamira hiyo inatekelezwa kupitia Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Wanawake, Amani na Usalama wa mwaka 2025–2029 uliozinduliwa Agosti 2025, ambao unalenga kuunganisha taasisi za Serikali na wadau wengine katika kuhakikisha ajenda hiyo inatekelezwa katika ngazi zote.
Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa ICGLR kutekeleza Azimio la Dar es Salaam na Mpango wa Pili wa Kikanda wa Wanawake, Amani na Usalama wa mwaka 2026–2030, akitoa wito kwa nchi hizo kudumisha mshikamano na kugeuza makubaliano yaliyofikiwa kuwa vitendo vitakavyoleta amani, usalama na maendeleo katika ukanda wa Maziwa Makuu

