Sumbawanga, Rukwa

Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa ni miongoni mwa miji yenye mtandao mkubwa wa barabara za lami nchini hivyo kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa manispaa hiyo na mkoa kwa ujumla.

Uwepo wa barabara hizo sio tu unachochea ukuaji wa kiuchumi kwa wakazi wake lakini pia umebadilisha mandhari ya mji huo na kuufanya wa kisasa na kuwa kivutio hasa kwa wageni wanaotembelea katika manispaa hiyo.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Rukwa Mhandisi Chacha Mwita Moseti amesema hali ya barabara katika mji wa Sumbawanga kwa sasa ni nzuri kwani kati ya barabara za lami km 62 ambazo zipo katika Mkoa wa Rukwa asilimia 98 ya barabara hizo ambazo ni sawa na km 60.7 zipo katika Manispaa ya Sumbawanga.

“Kwa Sasa mazingira yamependeza, mji una barabara za lami za kutosha na barabara zote zimewekwa taa ambapo wananchi sasa wanaweza kupita bila kujali sasa ni muda gani, iwe usiku au mchana wanapita bila hofu yeyote” amesema Mhandisi Moseti.

Ameongeza kuwa kutokana na uwepo wa mtandao huo wa barabara za lami hata huduma za kijamii na kiuchumi kama afya, elimu na masoko zinafikika kwa urahisi kwani maeneo ambayo yalikuwa hayafikiki sasa yanafikika muda wote wa saa 24 hivyo zimechangia kuinua hali ya maisha kwa wananchi wa mji wa Sumbawanga.

Akielezea hali ya mtandao wa barabara kimkoa, Mhandisi Moseti amesema asilimia 72.4 ya mtandao wa barabara katika Mkoa wa Rukwa zinapitika na bado wanaendelea na matengenezo ambapo kwa mwaka huu wa fedha 2026/27 wametengewa bajeti ya shilingi bilioni 12.4.

” Tumeshafanya manunuzi asilimia 60 ya bajeti yetu ambapo makandarasi wameshapatikana na wapo ‘site’ wanaendelea na utekelezaji wa kazi.” amefafanua.

Kuhusu utayari wa kukabiliana na mvua za el-nino Mhandisi Moseti amesema wamejiandaa vizuri kwani mpaka sasa wameshazibua mitaro katika maeneo yao yote sambamba na kusafisha mito ili kuruhusu maji yaweze kupita bila kikwazo chochote, pamoja na kubaini maeneo hatarishi ili kuweza kuchukua hatua stahiki endapo changamoto itatokea.

Kwa upande Bw. Juma Abubakar Juma ambaye ni dereva wa bajaji mkazi wa Majengo, Manispaa ya Sumbawanga ameishukuru serikali kwa kujenga barabara za lami katika manispaa ya Sumbawanga kwani imefanya kazi yake kuwa rahisi ambapo kwa sasa anaweza kuwasafirisha abiria wake kwenda mjini na kurudi kwa wakati, huku matengenezo ya mara kwa mara ya chombo chake yakiwa yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Naye Bi Salafina Kilapi mkazi wa Majengo amesema hapo awali walikuwa na changamoto kubwa ya usafiri kutokana na barabara mbovu lakini baada ya ujenzi wa barabara ya lami Sasa Hali ya usafiri imekuwa nzuri. 

Kwa mujibu wa Bi. Salafina hali ya usalama katika mtaa wao ilikuwa ni tete lakini baada ya kujengwa barabara ya lami na kuwekwa taa, sasa mtaa wao umekuwa na usalama wa kutosha na wapo huru na maisha yao.