Jumla ya tembo 99 wamefanikiwa kuondolewa katika maeneo mbalimbali ya makazi ya wananchi na mashambani wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, kufuatia operesheni maalumu ya siku saba ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu iliyotekelezwa kuanzia Oktoba 26 hadi Novemba 1, 2026.

Mafanikio hayo yamebainishwa wakati wa tathmini ya operesheni hiyo, ambapo taasisi za uhifadhi zilizoshiriki zikiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa operesheni hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, akiwa pamoja na Kamati ya Usalama ya Wilaya.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amesema operesheni hiyo imefanyika kwa mafanikio makubwa, huku akisisitiza kuwa mikakati ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ikiwemo operesheni zitaendelea kutekelezwa ili kulinda usalama wa wananchi na mali zao.

Kwa upande wao, viongozi wa taasisi za uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wameeleza kuwa mpango wa muda mrefu wa kupunguza migogoro kati ya wananchi na wanyamapori ni kuhakikisha upatikanaji wa maji ndani ya hifadhi kwa kuchimba visima virefu na kujenga mabwawa ya maji, ili wanyamapori hao wasilazimike kutoka nje ya hifadhi kutafuta huduma hiyo.

Katika taarifa ya tathmini inaeleza kuwa Kata ya Maore, Kisiwani na Ndungu tembo 19 walidhibitiwa, Makanya na Hedaru 50, Ruvu tembo 27 na Kata ya Njoro tembo 3 huku jumla ikiwa ni tembo 99 waliodhibitiwa na kurejeshwa hifadhini.

Pia wameeleza kuwa operesheni hizo zitaendelea kufanyika mara kwa mara huku wananchi wakisisitizwa kuendelea kutoa taarifa za haraka pindi wanapoona wanyamapori wakali na waharibifu wakiingia katika maeneo ya makazi au mashambani, ili taasisi za uhifadhi ziweze kuchukua hatua kwa wakati na kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.

Nao baadhi ya wananchi wameishukuru Serikali kwa kutekeleza operesheni hiyo, wakieleza kuwa hatua hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa katika kuimarisha usalama wao na kulinda shughuli zao za kilimo dhidi ya uharibifu na hasara zinazosababishwa na tembo.