Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kutambua mchango mkubwa wa wenye viwanda na wafanyabiashara wadogo na wa Kati katika kukuza uchumi na kuongeza mapato ya Serikali, hivyo itaendelea kushirikiana nao kwa kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha biashara kukua na kuimarika
Akizungumza leo Jijini Dodoma Novemba 2, 2026, katika maonesho yanayoelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda na sera ya Maendeleo ya Jasiriamali ndogo na za kati, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Paul John Walalaze, amesema maendeleo ya viwanda na ukuaji wa biashara ni miongoni mwa mambo muhimu yatakayochochea ongezeko la mapato ya Serikali.
Walalaze amesema kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara nchini kupitia maboresho mbalimbali yanayolenga kurahisisha shughuli za biashara, kuimarisha sekta ya viwanda na kuwezesha wafanyabiashara wadogo kupata mitaji na fursa za kukuza shughuli zao.
Amesema mwaka wa fedha 2025/26 ni wa kwanza katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, ambayo imeweka msisitizo katika maendeleo ya viwanda na sekta binafsi kama nguzo muhimu za kufikia malengo ya uchumi wa taifa.
Bw. Walalaze ameeleza kuwa kuimarika kwa mazingira ya biashara kutaiwezesha TRA kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuchangia kufikiwa kwa azma ya Tanzania kuwa na uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Amesema TRA ina lengo kuu la kukusanya Shilingi trilioni 42 katika mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni ongezeko kutoka Shilingi trilioni 37 zilizokusanywa katika mwaka wa fedha uliopita, huku ikiendelea kuimarisha ushirikiano na sekta ya viwanda na wafanyabiashara ili kukuza mapato ya Serikali.
Aidha, amewataka wafanyabiashara wote nchini kuhakikisha wanatoa risiti za mauzo kwa wateja wao, huku wananchi wanaonunua bidhaa katika viwanda na kwa wafanyabiashara lwadogo wakihimizwa kudai risiti kila wanapofanya manunuzi.
Amesisitiza kuwa risiti ni sehemu muhimu ya utambuzi na usimamizi wa kodi za Serikali, hivyo matumiz i yake sahihi yatachangia kuongeza mapato yanayotumika kugharamia huduma za kijamii na miradi ya maendeleo nchini.
