Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata yametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria kwa kupatanisha na kusuluhisha migogoro ya ndoa badala ya kujichukulia mamlaka ya kutoa maamuzi kama mahakama.

Wito huo umetolewa na Mwanasheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, John Bundala, Nov 2,2026 wakati akitoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wajumbe wa Baraza la Usuluhishi la Kata ya Mkuza, Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, kuhusu wajibu na taratibu za kushughulikia migogoro ya ndoa.

Bundala amesema wajibu wa mabaraza hayo ni kuwasaidia wanandoa kufikia maridhiano kupitia usuluhishi, na kwamba pale yanaposhindwa kutatua mgogoro wowote yanapaswa kutumia fomu maalumu walizoachiwa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid), ili kuwaelekeza wahusika kwenye mabaraza ya ngazi ya wilaya kwa hatua zaidi za kisheria na maamuzi.

Amesema elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wajumbe kuhusu sheria, namna ya kuendesha vikao na taratibu sahihi za kushughulikia migogoro, huku akisisitiza umuhimu wa kutenda haki na kuepuka kuvuka mipaka ya mamlaka yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Usuluhishi la Kata ya Mkuza, Amin Juma, amesema wamepata elimu iliyowaongezea uelewa katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu yao, jambo litakalowasaidia kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Hadi sasa, zaidi ya Mabaraza matano ya Usuluhishi katika kata mbalimbali yamefikiwa na kampeni hiyo, ambapo wajumbe wamepatiwa elimu ya sheria na taratibu za usuluhishi, sambamba na huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wa Kata ya Mkuza kwa kusikiliza kero zao na kuwasaidia kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.