Serikali imeendelea kuweka uzito katika kuboresha miundombinu na mifumo ya utoaji wa huduma za afya nchini, ambapo mkoani Mbeya zoezi la tathmini ya ubora wa huduma kwa mfumo wa utoaji nyota (Star Rating Assessment) limeendelea kushika kasi leo Novemba 2026 kote mkoani humo.
Zoezi hilo la kimkakati linatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu wa afya kutoka Wizara ya Afya, TAMISEMI na timu za afya ngazi ya mkoa na wilaya Mbeya.
kiongozi wa timu ya wataalam wao Dkt Mbwana Martine amesema kuwa Tathmini hii imelenga maeneo yote kwa kuhusisha Halmashauri zote saba za Mbeya ambazo ni Jiji la Mbeya, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya (Vijijini), Rungwe, Busokelo, Kyela, Chunya, na Mbarali.
Amesema kuwa Maboresho haya yanakuja wakati muafaka ili kuhakikisha miundombinu hiyo inaenda sambamba na mahitaji ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Bima ya Afya kwa Wote.
Mfumo huo wa bima ulizinduliwa rasmi tarehe 22 Oktoba, 2026 mkoani Mtwara na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ikiwa ni hatua kubwa kuelekea kuhakikisha kila mwananchi anapata matibabu bila vikwazo vya kifedha.
Ameeleza kuwa Kufanyika kwa tathmini hiyo mkoani Mbeya ni mwendelezo wa jitihada za makusudi zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Afya ikishirikiana bega kwa bega na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na unalenga kutimiza kwa vitendo malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayoweka msisitizo mkubwa wa kisheria na kijamii katika uboreshaji wa utoaji wa huduma bora, salama, na za kuaminika za afya kwa wananchi wote.

