Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam

Tanzania imeendelea kupiga hatua katika mapambano dhidi ya malaria na kuingia katika kundi la kijani kwenye mfumo wa tathmini wa Malaria Scorecard, unaopima maendeleo ya udhibiti wa ugonjwa huo, licha ya baadhi ya mikoa kuendelea kuwa na maambukizi ya kati ya asilimia saba hadi 12.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, amesema hayo leo Novemba 2, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wataalamu wa malaria kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika. 

“Muungano wa Viongozi wa Afrika Dhidi ya Malaria (ALMA), kwa kushirikiana na Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) na RBM Partnership to End Malaria, unaunganisha nchi za Afrika katika kuweka mikakati ya pamoja ya kupunguza na kutokomeza malaria, hususan maeneo yenye maambukizi makubwa,” amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema kuwa mkutano huo unalenga kuandaa Ripoti ya Maendeleo ya Malaria Afrika itakayowasilishwa kwa Wakuu wa Nchi na Serikali katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Afrika Januari 2027, kwa ajili ya kujadili mafanikio, changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kutokomeza malaria.

“Maandalizi ya mkutano huu nchini ni sehemu ya kutekeleza dhamira iliyooneshwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa Februari mwaka huu ambapo viongozi walitoa ahadi ya kugharamia, kuongoza na kumaliza mapambano dhidi ya malaria,” amesema Dkt. Magembe

Pia, Dkt. Magembe amesisitiza umuhimu wa ripoti hiyo kutumia takwimu sahihi na za wakati ili kusaidia viongozi kuelekeza rasilimali katika maeneo yatakayozalisha matokeo makubwa, akibainisha kuwa ufadhili wa ndani unapaswa kupewa kipaumbele na kusaidiwa na ufadhili wa nje.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Afya na Masuala ya Kibinadamu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Prof. Julio Rakotonirina, amesema maendeleo ya mapambano dhidi ya malaria barani Afrika yanaendelea ikiwemo usugu wa dawa na viuatilifu pamoja na mabadiliko ya tabianchi,

Mwisho, Dkt. Magembe amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kudhibiti mazalia ya mbu kwa kutunza mazingira, kufyeka vichaka, kuzibua mitaro na kuondoa maji yaliyotuama pamoja na kuwasisitiza wananchi kupima kabla ya kutumia dawa, kuepuka matumizi holela ya dawa na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.