Mkuu wa mkoa wa Rukwa Charles Makongoro Nyerere wakati akizungumza na wananchi, viongozi wa serikali , viongozi wa dini katika uzinduzi wa bima ya afya kwa wote Manispaa ya Sumbawanga.

Mkuu wa mkoa wakati akimkabidhi Mwananchi kadi ya bima ya afya ikiwa ni uzinduzi rasmi wa usajili wa bima ya afya kwa wote.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa bima ya afya kwa wote iliyofanyika Manispaa ya Sumbawanga

…………..

Na Neema Mtuka, Sumbawanga

Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wameelezea matumaini mapya baada ya kuzinduliwa kwa Awamu ya Pili ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, wakisema sasa wamepata unafuu wa gharama za matibabu zilizokuwa zikiwakwamisha.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 2 , 2026 kabla ya uzinduzi huo, mmoja wa wananchi aliyenufaika na awamu ya kwanza Anna Stella Maufi amesema, “Kabla ya bima hii, tulikuwa tukishindwa kwenda hospitali kwa kuogopa gharama. Sasa baada ya kupata kadi, tunatibiwa bila wasiwasi.”

Katika uzinduzi huo uliofanyika leo mjini Sumbawanga, jumla ya kaya 10 zimekabidhiwa kadi za Bima ya Afya kwa Wote zenye thamani ya shilingi laki moja na elfu hamsini (150,000) kwa kila kaya, ikiwa ni ishara ya kuanza kwa usajili rasmi.

Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Charles Makongoro Nyerere, ambaye amezindua rasmi zoezi hilo na kuwataka wananchi wa Rukwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.

Makongoro amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka afya ya wananchi kama kipaumbele cha kwanza, na mpango huo ni utekelezaji wa dhamira ya kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma bora ya afya bila kujali kipato chake.

“Afya bora ni msingi wa maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla. Nawasihi wananchi wote wa Rukwa, kuanzia Sumbawanga, Kalambo, Nkasi na Laela, mjitokeze kuchangamkia fursa hii,” amesema Makongoro Nyerere.

Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Rukwa, Donald Malunda, amesema wamejipanga kikamilifu kutekeleza zoezi hilo kwa kuanza na ngazi ya kaya.

Malunda amesema mfumo umeboreshwa ili kuhakikisha usajili unafanyika kwa haraka na kadi zinatolewa kwa wakati, huku akibainisha kuwa kaya moja italipiwa kwa pamoja na kunufaika wote.

“Katika awamu hii ya pili, tumejipanga kuanza na kaya kama kitovu cha usajili. Lengo letu ni kuhakikisha hakuna kaya inayobaki nyuma katika kupata huduma ya bima ya afya,” amesema Malunda.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa, wakiwemo wataalamu wa afya, viongozi wa dini na wananchi.