Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam

Simba SC na Yanga SC zimejikuta katika mazingira yanayoweza kuchochea kisasi cha soka baada ya kupangwa katika makundi yenye wapinzani ambao wana historia ya kukutana nao katika mashindano ya kimataifa ligi ya Mabigwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Katika droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyofanyika jijini Cairo, Misri, Oktoba 28, 2026, Yanga imepangwa Kundi B, huku Simba ikiangukia Kundi C, hali inayozipa timu hizo za Tanzania changamoto ya kupambana na wapinzani wenye uzoefu katika mashindano hayo.

Kwa Yanga, macho yataelekezwa zaidi katika mechi dhidi ya Zamalek ya Misri na MC Alger ya Algeria, ambazo zimewahi kuipa wakati mgumu katika mashindano ya soka la Afrika.

Simba, kwa upande wake, italazimika kukabiliana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini na RS Berkane ya Morocco, timu ambazo zimewahi kuizima ndoto yake ya kutwaa ubingwa katika mashindano ya kimataifa.

Hali hiyo inazifanya mechi za hatua ya makundi kuwa zaidi ya vita ya kutafuta pointi, kwani kila upande utakuwa na nafasi ya kurekebisha historia na kuthibitisha uwezo wake mbele ya wapinzani ambao tayari wanaifahamu.

YANGA SC KULIPA KISASI

Yanga ina kumbukumbu ngumu dhidi ya Zamalek, ambayo imewahi kuiondoa katika mashindano ya Afrika. Mara ya kwanza timu hizo kukutana ilikuwa mwaka 2000, katika raundi ya kwanza ya Kombe la Washindi Afrika, ambapo Yanga ilitolewa kwa jumla ya mabao 5-1.

Miaka 12 baadaye, timu hizo zilikutana tena katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hata katika pambano hilo, Yanga ilishindwa kusonga mbele baada ya kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1 na wababe hao wa Misri.

Historia hiyo inaweka msisitizo katika umuhimu wa Yanga kujiandaa kwa umakini, hasa ikizingatiwa kuwa mchezo dhidi ya Zamalek unaweza kuwa kipimo cha uwezo wake wa kupambana na timu zenye uzoefu mkubwa katika mashindano ya bara.

Mbali na Zamalek, MC Alger ni mpinzani mwingine ambaye Yanga itahitaji kumkabili kwa tahadhari kutokana na matokeo walivyokutana hivi karibuni.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024/2025. Katika mchezo uliopigwa jijini Dar es Salaam, zilitoka sare ya bila kufungana, kabla ya MC Alger kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa marudiano nchini Algeria.

Matokeo hayo yanaifanya mechi ijayo kuwa fursa kwa Yanga kutafuta matokeo tofauti, huku ikilenga kutumia uzoefu iliyopata katika michezo walikutana nao.

Hata hivyo, si kila historia ya Yanga katika mashindano ya Afrika imekuwa ya kupoteza dhidi ya wapinzani wake. Msimu wa 2022/2023, ilikutana na Club Africain ya Tunisia katika raundi ya mchujo ya Kombe la Shirikisho Afrika na kufanikiwa kusonga mbele.

Yanga ilianza kwa kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani, kabla ya kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini na kufuzu kwa hatua iliyofuata.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa timu hiyo ina uwezo wa kupata matokeo mazuri hata inapocheza kwenye viwanja vya wapinzani.

SIMBA SC KUANDIKA HISTORIA MPYA.

Kwa upande wa Simba, mtihani mkubwa unahusisha Orlando Pirates na RS Berkane, ambazo zimewahi kuikwamisha katika harakati zake za kutafuta mafanikio ya kimataifa.

Simba ina kumbukumbu ya kukosa nafasi ya kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kukutana na RS Berkane katika fainali ya msimu wa 2024/2025.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Morocco, Simba ilipoteza kwa mabao 2-0, kabla ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa marudiano uliofanyika Zanzibar. Matokeo hayo yaliipa RS Berkane ubingwa, huku Simba ikibaki na maumivu ya kukosa taji hilo.

Kukutana tena kwa timu hizo kunatoa nafasi kwa Simba kuonyesha maendeleo iliyopata tangu fainali hiyo na kupambana kupata matokeo yatakayoiweka katika nafasi nzuri ya kuendelea na safari yake ya kutafuta mafanikio Afrika.

Changamoto nyingine kwa Simba ni Orlando Pirates, ambayo iliiondoa katika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021/2022.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa nyumbani, Simba ilipata ushindi wa bao 1-0, lakini ikapoteza kwa matokeo kama hayo katika mchezo wa marudiano ugenini.

Timu hizo zililazimika kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, ambapo Orlando Pirates ilishinda kwa penalti 4-3 na kusonga mbele.

Historia hiyo inaonyesha jinsi pambano dhidi ya Orlando Pirates linavyoweza kuwa gumu, hasa kutokana na uwezo wa timu hiyo kupambana hadi dakika za mwisho na kutumia nafasi zinazojitokeza katika mechi zenye presha kubwa.

Kwa Simba, mechi hizo zitakuwa nafasi ya kubadilisha kumbukumbu za nyuma na kuonyesha kuwa ina uwezo wa kushindana na timu zenye historia kubwa katika soka la Afrika.

Tofauti na wapinzani wengine wenye historia ya kukutana na timu za Tanzania, Colombe Sport ni miongoni mwa timu mpya katinga hatua ya makundi.

Michezo ya ligi ya mabigwa barani Afrika hatua ya makundi inatarajia kutimua vumbi Novemba 27, 2026.