Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wameagiza upimaji ardhi wa Taasisi za Serikali kufanyika ili kupatikana kwa hati miliki na kuepuka uvamizi.
Madiwani hao wameazimia hayo kwenye kikao cha Baraza la lao lililofanyika makao makuu ya Wilaya hiyo mji mdogo wa Orkesumet.
Mjumbe wa kamati ya uchumi, ujenzi na mazingira Robert Melembuki amesoma maazimio hayo kwenye kikao cha Baraza hilo.
Robert amesema Mkurugenzi mtendaji anapaswa kuendeleza zoezi la upimaji wa taasisi za Serikali na maeneo yanayomilikiwa na Halmashauri hiyo.
Amesema upimaji ufanyike ili kuepuka uvamizi na kutoa hati miliki kwa maeneo hayo na kuwasilisha kwenye kikao kijacho cha Baraza la Madiwani.
Amesema kwenye wasilisho hilo anapaswa kubainisha idadi ya taasisi zilizopimwa hadi sasa na zilizobaki kwa majina.
“Mkurugenzi afanye mawasilaino na kamati ya kutatua migogoro ya ardhi iliyoundwa na Wizara ya Ardhi ili kufahamu lini watakuja kutatua migogoro ya ardhi kwani imekuwa sugu,” amesema Robert.
Pia, amesema Mkurugenzi mtendaji anapaswa kuendelea kuweka mikakati ya kulinda vyanzo vya asili vya maji (njoro) na kuondoa waliovamia vyanzo hivyo.
Amesema Mkurugenzi mtendaji kwa kushirikiana na RUWASA waweke mpango wa kutoa elimu kwa jamii ili waelewe umuhimu wa kutunza miundombinu ya vyanzo vya maji kwenye ngazi ya vijiji.
“Mkurugenzi mtendaji awasiliane na TARURA ili waweke mpango wa matengenezo ya barabara kwenye maeneo korofi kama korongo lililopo kata ya Emboreet, Endonyongijape, Shambarai na maeneo mengine.
