Na Mwandishi Wetu, WMTH – Libreville, Gabon 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), amesisitiza umuhimu wa kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika mipango ya maendeleo ya ujuzi wa kidijitali, hususan Akili Unde (AI), ili kuhakikisha wanapata fursa sawa katika uchumi wa kidijitali.

Mhe. Kairuki ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa Sita wa Kawaida wa Kamati Maalumu ya Kiufundi ya Umoja wa Afrika kuhusu Mawasiliano na TEHAMA (STC-CICT-6), unaofanyika tarehe 29–30 Oktoba 2026 jijini Libreville, Gabon.

Mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo “Africa’s Digital Future, Africa’s Voice: Advancing Innovation, Digital Inclusion and Shaping Africa’s Narrative” unalenga kuimarisha ushirikiano wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika kukuza ubunifu, ujumuishi wa kidijitali na nafasi ya Afrika katika maendeleo ya teknolojia, huku ukihimiza kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma.

Waziri Kairuki ameongeza kuwa ujumuishi huo unapaswa kuzingatiwa kuanzia uandaaji wa sera na programu hadi utekelezaji wa miradi, ikiwemo upatikanaji wa maudhui ya mafunzo, matumizi ya teknolojia saidizi na uundaji wa mifumo ya kidijitali inayofikika kwa watu wote.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha programu za uwezeshaji wa vijana na wanawake zinazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu ili nao wanufaike na fursa za mafunzo, ajira na ubunifu zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.

Katika mkutano huo, Tanzania imeunga mkono juhudi za kuimarisha miundombinu ya kidijitali ya kikanda, kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kuendeleza matumizi salama na yenye uwajibikaji ya teknolojia zinazoibuka.