Na Dennis Mlowe, Kilolo

WILAYA ya Kilolo mkoani Iringa imeweka historia baada ya kufanyika kwa kilele cha mbio za Kitonga Marathon 2026, zilizolenga kutangaza fursa za utalii, uwekezaji na uhifadhi wa mazingira, huku Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ikiahidi kushirikiana na halmashauri hiyo kukamilisha mpango wa kuanzisha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA).

Akizungumza katika kilele cha mbio hizo akiwa mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande, amesema Mlima Kitonga ambao kwa muda mrefu umekuwa ukihusishwa na ajali za barabarani sasa una nafasi ya kuwa kivutio cha utalii na chanzo cha fursa za kiuchumi kwa wananchi kupitia michezo na utalii wa asili.

Chande ameipongeza halmashauri kwa kuanzisha mbio hizo na kueleza kuwa Serikali iko tayari kutoa ushirikiano kuhakikisha mpango wa WMA unakamilika, akiahidi kulifikisha suala hilo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii ili wananchi wa Kilolo wanufaike na rasilimali za wanyamapori zilizopo katika maeneo yao.

Amesema Kilolo imebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba, misitu, hali nzuri ya hewa na vivutio mbalimbali vya asili vinavyoweza kuvutia wawekezaji na watalii kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Siwema H. Jumaa, amesema mbio hizo zimeandaliwa kwa ushirikiano wa wadau zaidi ya 73 kutoka taasisi za umma na binafsi, wakiongozwa na Exim Bank kama mdhamini mkuu, huku mashindano yakihusisha kilomita tano, 10, 21 na mbio za milimani (Trail Run).

Amesema zaidi ya washiriki 180 walishiriki mbio za Trail Run kwa kupanda Mlima Kitonga, hatua inayofungua fursa mpya ya utalii wa kupanda milima, huku maandalizi ya tukio hilo yakihusisha pia usafi wa mazingira, ugawaji wa mapipa 10 ya taka na mizinga 20 ya nyuki kwa vikundi vya vijana ili kuwawezesha kujipatia kipato na kushiriki katika uhifadhi wa mazingira.

Jumaa ameongeza kuwa halmashauri ilifanya bonanza la michezo katika kata mbalimbali na kutembelea kituo cha watoto wenye mahitaji maalumu cha Filipo kilichopo eneo la Image na Mbambali, Kata ya Ilula, kwa ajili ya kutoa msaada.

Ametaja baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo Kilolo kuwa ni Chui camp, maporomoko ya maji ya Idenda na Uluti, mapango ya Magombelena, eneo la Nyautwa katika Kijiji cha Masege pamoja na Kaburi la Nyundo lililopo Kata ya Lugalo, ambalo ni kumbukumbu ya kihistoria ya askari 300 wa Kijerumani waliozikwa eneo hilo.

Amesema halmashauri inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, ikiwemo mradi wa umwagiliaji wa Mbalanga wenye uwezo wa kuhudumia ekari 4,236, pamoja na kuweka mfumo wa kituo kimoja cha huduma kwa wawekezaji (One Stop Centre).

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Atupele Makibete, amesema wilaya hiyo imetenga zaidi ya ekari 21,000 kwa ajili ya uwekezaji, ambapo maeneo hayo yanajumuisha ardhi kwa ajili ya viwanda na kilimo cha chai, kahawa, matunda, miwa na mazao mengine.

Makibete amesema Kilolo ina fursa kubwa ya utalii kutokana na ukaribu wake na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, lakini changamoto za miundombinu zimekuwa zikifanya baadhi ya watalii kuelekea Morogoro badala ya kutumia njia ya Kilolo, hivyo kuiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kusaidia kuitangaza wilaya hiyo na kuvutia wawekezaji wakubwa.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Rashid Nzelemera, amesema kaulimbiu ya mbio hizo isemayo ‘Tunza Mazingira, Wekeza Kilolo’ inalenga kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na matumizi ya rasilimali kwa maendeleo ya wananchi.

Ameiomba Serikali kusaidia kuboresha barabara ya Mlima Kitonga ili kuimarisha usalama wa watumiaji wake na kuwezesha shughuli za utalii na michezo, huku akisisitiza umuhimu wa kukamilishwa kwa WMA ili wananchi wanufaike na uwepo wa wanyamapori badala ya kuwaona kama kikwazo cha maendeleo.

Katika matokeo ya mashindano hayo, kwa upande wa wanawake kilomita 21, mshindi wa tatu alikuwa Visa Arnold Mhalwa kutoka Iringa, akitumia saa moja, dakika 35 na sekunde 23, mshindi wa pili Dorcas Bonifaz Ilanda kutoka Arusha aliyetumia saa moja, dakika 31 na sekunde saba, huku mshindi wa kwanza Angelina Joseph kutoka Singida akitumia saa moja, dakika moja na sekunde 38.

Kwa upande wa wanaume kilomita 21, mshindi wa kwanza alikuwa Agustino Harry McAfee kutoka Babati, mkoani Manyara, aliyemaliza mbio hizo kwa saa moja, dakika sita na sekunde 31.

Kitonga Marathon 2026 imefanyika ikiwa na dhamira ya kuitangaza Kilolo kama eneo lenye fursa za uwekezaji, utalii wa michezo na utalii wa asili, huku wadau wakihimizwa kushirikiana katika kulinda mazingira na kukuza uchumi wa wananchi.