Ataka habari za vijijini zipewe kipaumbele, vyombo vya habari viimarishwe kiuchumi
Na Sophia Kingimali.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amewataka waandishi wa habari kurejesha nafasi yao ya kitaaluma katika jamii kwa kuandika habari zinazogusa maisha ya wananchi na kuibua changamoto zinazohitaji kutatuliwa.
Amesema jukumu la msingi la wanahabari ni kuhabarisha umma kwa weledi na kusimamia maslahi ya wananchi, hivyo kuna umuhimu wa kuboresha ubora wa habari ili kurejesha ushawishi wa vyombo vya habari katika jamii.
Msigwa ameyasema hayo leo Octoba 31,2026 Jijini Dodoma alipokutana na viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini (RUJAT) na wadau mbalimbali wa sekta ya habari,wakati akifungua Kongamano la mwaka la tathimini ya huduma za habari na mawasiliano vijijini nchini Tanzania ambapo amesisitiza umuhimu wa kufanya utafiti kubaini sababu zinazowafanya wananchi kupunguza ufuatiliaji wa vyombo vya habari.
Amesema mwandishi wa habari anapaswa kutekeleza jukumu lake kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi badala ya kuacha nafasi ya kitaaluma ya kuhabarisha umma ichukuliwe na makundi yenye ajenda au malengo maalumu.
“Tusipokubali jukumu la kitaaluma la wanahabari lifanywe na wanaharakati tunapoteza umuhimu wetu na tunawanyima haki sahihi wananchi,” amesema.
Katika hatua nyingine, ameipongeza RUJAT kwa kuanzisha jukwaa maalumu la kuimarisha upatikanaji wa habari za vijijini, akisema takribani asilimia 65 ya Watanzania wanaishi vijijini, huku zaidi ya asilimia 80 ya vyombo vya habari vikiwa mijini kwa mujibu wa takwimu za miaka mitano iliyopita.
Amesema hali hiyo imechangia wananchi wengi wa vijijini kukosa habari zinazohusu mazingira na mahitaji yao, hivyo akawataka waandishi kutumia jukwaa hilo kuwafikia wananchi na kuibua changamoto zinazohitaji ufumbuzi.
“Hatimaye sasa sisi waandishi wa habari tumeamua kwa dhati kuwafikia asilimia 65 ya Watanzania wanaoishi vijijini,” alisema.
Aidha, amewataka waandishi kuimarisha uchumi wa vyombo vya habari na kujenga uwezo wao wa kiuchumi ili kulinda uhuru na weledi wa taaluma hiyo, akisema utegemezi wa fedha kutoka kwa watu au taasisi zenye maslahi maalumu unaweza kuathiri uhuru wa uandishi.
“Ni lazima tutengeneze mipango mahususi itakayoviwezesha vyombo vyetu vya habari na waandishi wa habari kuwa na nguvu za kiuchumi. Tusipofanya hivyo tunasababisha nchi yetu iwe na waandishi wa habari dhaifu na vyombo vya habari dhaifu,” alisema.
Kwa upande wake CHAMA cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT) Prosper Kwigize,amesema chama kimeweka mkakati wa kuimarisha uandishi wa habari unaozingatia changamoto na mahitaji ya wananchi wa vijijini, kwa lengo la kuhakikisha sauti zao zinasikika, zinathaminiwa na habari zinazochapishwa zinachochea matokeo katika jamii.
Amesema chama hicho kilianzishwa mwaka 2020 na waandishi wa habari 20 waliokutana Dodoma, baada ya kubaini umuhimu wa kuwa na mfumo maalumu wa kuhabarisha wananchi wa vijijini kama ilivyo katika baadhi ya nchi nyingine.
Amesema wazo hilo lilitokana na kujifunza mifumo ya uandishi wa habari za vijijini katika nchi nyingine na kuona umuhimu wa Tanzania kuwa na chama kinacholenga eneo hilo, huku mawazo ya kuanzisha taasisi hiyo yakibebwa na waandishi kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam, Kigoma, Katavi, Morogoro, Iringa, Shinyanga, Mtwara, Mara na Simiyu.

