Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali mkoani Arusha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa na kuwaandaa wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutoa maoni na mapendekezo kuhusu rasimu hiyo.

Zoezi hilo lililofanyika leo, Oktoba 31, 2026, na kufunguliwa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Vicent Kayombo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mhe. CPA Amos Makalla, likiwakutanisha viongozi wa Serikali ya Mkoa na Wilaya, wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, taasisi za dini, mashirika ya kiraia pamoja na makundi maalumu ya kijamii, yakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Kupitia zoezi hilo, washiriki wamepata fursa ya kufahamu kuhusu Fungamano la Kisiasa la EAC, pamoja na hatua mbalimbali za mchakato wa kulianzisha. Elimu hiyo inalenga kuwawezesha wadau kuandaa masuala watakayohitaji yajumuishwe kwenye rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa na kujiandaa kutoa maoni na mapendekezo yao wakati mchakato rasmi wa ukusanyaji wa maoni utakapoanza.

Ushirikishwaji wa makundi mbalimbali ya kijamii ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Tanzania kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na fursa ya kushiriki katika mchakato huo, kwa kuzingatia kuwa maoni ya wadau ni muhimu katika kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mustakabali wa ujumuishaji wa kikanda na hatua za kuelekea Fungamano la Kisiasa la EAC.

Ujumbe wa Wizara katika zoezi hilo uliongozwa na Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Bi. Mwanamridu Amiry Jumaa.